
MWILI wa aliyekuwa mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Deutsche Welle (DW) nchini Ujerumani, Isaac Muyenjwa Gamba umeagwa katika ibada ya kuaga mwili huo iliyofanyika leo Jumatano, Oktoba 31, 2018 nyumbani kwao, Bunda mkoani Mara.

Baada ya ibada maalum ya kuaga, mwili wake ulipelekwa kwenye makaburi hayo ya familia yaliyopo Kijiji cha Wanyere, Kata ya Wanyere nje kidogo na mji huo wa Bunda ambako amezikwa.

Mamia ya waombolezaji wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili ambaye amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, Katibu Mkuu wa Chadema -Zanzibar, Salum Mwalimu na wengine wamejitokeza na kuungana na wanafamilia pamoja na waombolezaji kuzika mwili wa mkongwe huyo katika tasnia ya habari.

Weninge ni wanahabari wenzake, marafiki wa marehemu ambao baadhi yao wamesafiri kutoka Ujerumani akiwemo Sudi Mnyete, na wengine waliotoka Dar es Salaam na Mwanza wakiwemo mtangazaji wa TBC Taifa, Sam Mahela, Mkurugenzi wa Redio One, Deogratias Rweyunga na wengine.

Akizungumzia msiba wa Gamba, Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili amesma kuwa kifo cha hicho kiwe funzo kwa Watanzania waishio ughaibuni kuwa wanapaswa kuiga mfano wake wa yale aliyoyafanya akiwa nchini ujerumani ya kuhabarisha umma kuendana na taaruma yake.

Aidha, Bupilipili ameushukuru uongozi wote wa DW kwa kufanikisha shughuli zote za kuuleta mwili wa marehemu hadi kufika mjini Bunda na watu wote waliohakikisha mwili huo unafika salaama na kuwafariji familia.

Gamba alikutwa akiwa amefariki chumbani kwake Alhamisi, Oktoba 18, mwaka huu, jijini Bonn nchini Ujerumani alikokuwa akifanya kazi zake.

Baada ya uchunguzi wa hospitali nchini Ujerumani, imegundulika kuwa kilichosababisha kifo chake ni kuvuja kwa damu kwenye ubongo (Brain Hemorrhage) yaani presha ya damu.



PICHA NA DENIS MTIMA | GPL