
STAA wa Bongo Fleva, Diamond Platinumz ameshindwa kujizuia na kuonyesha kufarijika baada ya msanii mwenzake ambaye aliwahi kumshirikisha kwenye moja ya ngoma zake ‘Nitarejea’, Hawa Mayoka ‘Hawa wa Nitarejea’ afya yake kuanza kuimarika na kuonyesha tabasamu tofauti na mwanzo wakati anapelekwa India kutibiwa.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Diamond ameandika ujumbe na kusema angependa kusikia wazo zuri la biashara kutoka kwa mwanadada huyo ili amuweze, akitoka kwenye matibabu aanzishe biashara zake mwenyewe zitakazomwezesha kumudu maisha yake na kujiongezea kipato.

Diamond ameandika; Nafarijika kuona unatabasamu sasa, nitafurahi kusikia wazo zuri la biashara toka kwako nikuwezeshe 🙏🏻 #HawaIsSmilingNow”

Hivi karibuni Diamond alijitolea kumpeleka Hawa nchini India kwa matibabu yatakayogharimu milioni 50 ya ugonjwa uliothibitishwa na madaktari hapa Bongo kuwa ni ini kuwa na tatizo lakini alipofika huko aligundulika kuwa ana tatizo la moyo na kufanyiwa upasuaji.
