Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewaapisha Mawaziri wawili na Naibu Mawaziri wanne ambao aliwateua Jumamosi ya Novemba 10,2018 kufuatia mabadiliko madogo aliyoyafanya katika baraza la mawaziri.
Katika vipapo hivyo, vilivyofanyika leo Jumatatu Novemba 12, 2018 Ikulu jijini Dar es salaam, aliyeanza ni Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Joseph Kakunda na kufuatiwa na Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga.
Wakafuata manaibu waziri ambao ni Mary Mwanjelwa (ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma), Costantine Kanyasu (Maliasili na Utalii), Innocent Bashungwa (Kilimo) na hatimaye Mwita Waitara (Tamisemi). Katika halfa hiyo pia ameapishwa Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha sheria Jaji Januari Msofe.

Akizungumza wakati akiwaapisha viongozi hao, Magufuli alisema;
“Sekta ya Kilimo na Viwanda ni sekta nyeti na mara nyingi nimekuwa nikigombana na Waziri Mkuu nikimuuliza mbona hiki hakiendi? Mara nyingine nampigia simu saa 8 usiku nikimtuma huku na huku kwasababu ndio kiranja wa Mawaziri.
“Limetokea suala la Kahawa nilimtuma Waziri Mkuu akaenda kulishughulikia. Tena wengine wanaovuka mpaka kwenda kuuza Kahawa wanatokea kwa Waziri Mwijage, nikajiuliza au ameegemea kwenye Viwanda amesahau Biashara?
“Kuna kiwanda kilikuwa kimekaa bila ya uzalishaji nikamtuma Waziri Mkuu akaenda kutatua, wakati mwingine nampigia simu usiku wa manane ninamuagia. Mpaka nikamwambia sasa nitakufanya uwe Waziri wa Viwanda au Kilimo.

“Mkurugenzi wa TANTRADE hajui kama anatakiwa kutafuta masoko ya mazao yetu au yeye anasubiri tarehe 1 mwezi wa 7 ili afungue maonesho ya saba saba tu? Mkurugenzi wa TANTRADE anasubiri kupokea viingilio vya maonesho ya saba saba.
“Niliowateuwa mkaanze kufanya kazi leo. Tatizo hamfanyi kazi kwa kushirikiana, nendeni mkaanzishe coordination. Benki ya Wakulima watatoa fedha na Jeshi litaichukua Korosho, hakuna itakayoibiwa mimi nawajua. Jeshi likabangue kwa namna watayoona inafaa,” alisema Magufuli.