×

DAKTARI: AFYA YA JOKATE HATARINI

IMEVUJA! Miongoni mwa Wakuu wa Wilaya (ma-DC) wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Pombe Magufuli ‘JPM’ wanaochapa kazi vilivyo, yumo Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, Jokate Urban Mwegelo (31), Risasi Jumamosi limedokezwa.  Jokate aliteuliwa na Rais Magufuli kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mwezi Julai, mwaka huu ambapo mpaka sasa ameshafanya mambo makubwa kwa watu wa wilaya yake. Kufuatia uchapaji kazi huo uliotukuka, daktari ameeleza hatari ya kiafya anayokumbana nayo mwanadada huyo.

KABLA YA DAKTARI

Kwa mujibu wa watu wanaofanya kazi kwa ukaribu na Jokate, mrembo huyo amekuwa mstari wa mbele kutembea na ‘kuparangana’ nje ya ofisi, kuona na kushiriki miradi mbalimbali ya kimaendeleo kwa vitendo kwenye wilaya yake hiyo. “Amekuwa akishiriki kwa vitendo kwenye shughuli za huduma za kijamii kama sekta ya afya, elimu, maji na nyinginezo. “Hii yote anafanya hivyo ili kujua namna huduma zinavyotolewa na mamlaka husika zilizo chini yake kwa kushirikiana na jamii kama kweli jamii inaridhika na huduma hizo katika harakati zake za kuijenga Kisarawe mpya.

ANATUMIA MUDA MWINGI

“Kiukweli mheshimiwa anatumia muda wake mwingi sana kushiriki kwa vitengo shughuli za ujenzi wa vitu mbalimbali yakiwemo madarasa ambapo anaingia kazini na kubeba matofali na mchanga kama alivyofanya kwa Shule ya Msingi ya Marui Mipera (Kisarawe). “Mbali na shughuli hiyo pia alishiriki kwa mikono yake kuchimba kisima cha maji kwa ajili ya kutatua kero ya muda mrefu ya maji katika eneo hilo la Marui hivi karibuni.

ANAZUNGUKA TU

“Kama hiyo haitoshi, DC Jokate amekuwa akizunguka kwenye shule zote za Kisarawe kuanzia za msingi hadi sekondari na huko kote anafanya kazi za shurba za kutumia nguvu na kutokwa na jasho.

“Ukifuatilia ratiba yake, hadi siku inaisha, kwa mtu aliyekuwa hajishughulishi na kazi ngumu kama walivyo warembo wengi wa mjini, basi Jokate anakuwa amechoka kwelikweli,” kilisema chanzo hicho ambacho kinafanya kazi chini ya DC Jokate na kuongeza: “Mbali na shughuli za huduma kwa jamii, lakini Jokate anafanya kampeni na juhudi kubwa katika ujenzi wa mazingira rafiki kwa wawekezaji wadogo na wakubwa, ikiwemo kampeni ya ujenzi wa miundombinu wezeshi ya uchumi kama umeme, barabara na maji.

“Ukiacha kazi za mikono na kutembelea miradi, pia anafanya vikao na wawekezaji na kujadili changamoto mbalimbali na namna bora ya kuboresha na kusimamia miundombinu wezeshi kwa uwekezaji wenye tija kwenye wilaya yake ya Kisarawe. “Bila kusahau, pia Jokate ana kampeni kubwa ya ‘Tokomeza Ziro Kisarawe’ ambayo amekuwa akiifanya wilayani kwake kwa kutembelea shule moja baada ya nyingine kuhakikisha anaongeza hamasa ya ufaulu katika mitihani ya kidato cha nne na sita hivyo kama ni kuchoka, basi anachoka mno.”

DAKTARI SASA

Akizungumzia hali hiyo, daktari maarufu jijini Dar, Dk Godfrey Charles ‘Dk Chale’ alisema kuwa, kwa uchapaji kazi huo wa Jokate yupo kwenye hatari ya kukutana na hali ambayo kitaalam huitwa muscle fatigue au physical fatigue. Alieleza kuwa, fatique ni hali inayojitokeza mwilini pale misuli ya mwili inapofanyishwa kazi kupita kiwango chake.

“Kujitokeza kwa uchovu unaoambatana na maumivu ni njia mojawapo ya mwili kujihami na kukupa ishara kuwa viungo vya mwili ikiwamo misuli imetumika kupita kiasi. “Uchovu unasababisha misuli ya mwili kukosa nguvu kama ilivyo kawaida yake. Tatizo hili linaweza kuambatana na maumivu yanayoweza kuwa ya wastani mpaka kuwa makali.

“Hisia za uchovu huweza kuhisiwa zaidi katika maeneo ya maungio (joint), mgongoni, kiunoni, mapajani na magotini. “Mwathirika (kama Jokate) anaweza kuhisi pengine ana ugonjwa mkubwa kumbe ni uchovu wa viungo vya mwili tu.

“Uchovu unatokana na uwapo vitu vinavyoingilia hatua za utendani yaani kukunjuka na kujikunja kuwezesha matendo mbalimbali ikiwemo kukimbia, kuruka na kutembea. “Tatizo hili linaweza kusababishwa na mishipa ya fahamu kutosisimua vizuri misuli na uwepo wa mrundikano wa mabaki au taka-mwili baada ya seli kutumia sukari ya mwili kupita kiwango chake.

“Uchovu unaotokana na mwili kufanya kazi sana ni tatizo la muda tu ambalo linaweza kuisha endapo mambo mbalimbali yatafanyika. “Mtu anapokuwa na uchovu anahitajika kulala kati ya saa 6 hadi 8 bila usumbufu wowote ili kuepuka kukatika katika kwa usingizi. “Katika mazingira kama haya, mtu anahitaji  kupumzisha mwili katika maeneo yenye hewa safi ikiwemo ufukweni au maeneo ya wazi kwani mazingira ya hewa chafu yanachangia kuongeza uchovu zaidi.

“Anatakiwa kula mlo kamili ikiwemo vyakula vyenye protini, mboga za majani na matunda na vyakula vya wanga. “Lishe hii inasaidia kukurudishia nguvu iliyotumika, kurudisha akiba ya nishati katika misuli na kuwezesha ukarabati na uponaji wa vijeraha vya misuli. “Katika hali kama hiyo mtu mwenye fatique anapaswa kunywa maji lita 1.5 hadi 3 kabla ya kufanya mazoezi magumu na kufanya mazoezi mepesi kwa dakika kati ya 5 hadi 10 kabla ya kuanza mazoezi au shughuli za kila siku.

“Mtu kama huyo anatakiwa kufanya mazoezi ya viungo ya kunyoosha misuli ya mwili angalau kati ya dakika 10 hadi 15 huku akiwa katika mkao sahihi kimwili ili kuondoa uwezekano wa kujijeruhi misuli. “Mtu mwenye hali hii anatakiwa kufanya huduma ya usingaji au utomasaji (massage) kwa mafuta ya kuchua ili kulainisha misuli na kuwezesha damu kutirika kwa wingi katika misuli ili kuzidondoa taka-mwili au mabaki kirahisi katika misuli.

“Anatakiwa kuoga kwa maji ya uvuguvugu yanayotiririka kwa wingi au kuoga katika mabafu ya kisasa yenye kutoa mvuke wa joto. “Anatakiwa kuepuka mambo yatakayompa shinikizo la akili au kusababishia hisia hasi kwani yatamuongezea uchovu. Anapaswa kujichanganya katika mazingira ya burudani ili kumpa hisia chanya,” alisema daktari huyo, lakini akampongeza Jokate kwa kazi nzuri anayoifanya kwa wilaya yake ya Kisarawe.

JOKATE: NAUMWA

Katika hali ya kushtua, Risasi Jumamosi lilipomtafuta Jokate kwa njia ya simu alizungumza kwa unyonge akisema kuwa anaumwa. Hata hivyo, alipoulizwa anasumbuliwa na nini hakuwa tayari kusema nasi hatukuml-azimisha kwani ugonjwa ni siri ya mgonjwa na daktari.

KABLA YA UKUU WA WILAYA

Kabla ya kuteuliwa kuwa mkuu wa wilaya, Jokate alijulikana kama staa wa muziki, filamu, mitindo na urembo nchini.

STORI: Waandishi Wetu, Risasi Jumamosi