
MAANDIKO katika Qurani Tukufu yanasema mali zetu, wake zenu na watoto ni fitna kwenu; na kweli mali za mfanyabiashara tajiri Fakhi Mohamed Juma aliyefariki Agosti 13, mwaka huu, zinamfitisha duniani baba yake mzazi na mkewe.
Kivumbi na jasho cha kugombea mali zake kinatimka hivi sasa baada ya mwanamke mmoja anayedaiwa kuwa ni mke wa marehemu huyo aitwaye Tatu Mushi, mkazi wa Kitunda, jijini Dar es Salaam na mkwe wake (baba wa marehemu), Mohamed Juma, wote kwa pamoja kuibuka na kudai haki ya kumiliki mali za marehemu.
Kwa uchache marehemu Fakhi anadaiwa kuacha ghorofa mbili, nyumba mbili za kawaida, magari ya kutembelea na mabasi ya abiria maarufu kama daladala. Inadaiwa kuwa mvutano wa kumiliki mali kati ya ndugu, baba na mke wa marehemu haukusubiri matanga yaishe bali kila mmoja alianza kuchanga karata kivyake mapema ili kujiwekea misingi ya kupata haki ya urithi. Kutokana na kuwepo kwa mvutano, mambo yamekwenda kombo ambapo hivi sasa vyombo vya kutafsiri sheria viko kazini kuangalia uhalali wa nani anastahili kupewa urithi wa mali hizo za tajiri.

TUANZE NA MAELEZO YA MKE
Akizungumza na Amani kwa masikitiko, mke huyo wa marehemu alisema kuwa anasikitika kuona haki ya kumiliki mali inayumbishwa wakati yeye ni mke halali wa marehemu na kwamba amezaa naye watoto wawili ambao hivi sasa wanahitaji matunzo. “Mimi na mume wangu tulifunga ndoa mwaka 2002 na tulibahatika kupata watoto wawili, pia kuna mtoto mwingine nilimkuta naye alizaa na mwanamke mwingine ambaye kwa sasa yupo nchini Denmark kimasomo.

“Baadaye zikatokea changamoto kwenye ndoa yetu ikabidi mimi niondoke, kipindi mimi nimeondoka alioa mwanamke mwingine ambaye naye hakudumu sana akaondoka. “Baada ya hapo mume wangu alianza kuishi peke yake, wakati naondoka hakunipa talaka, alipoanza kupata mtihani wa kuugua akanipigia simu kuniomba turudiane na kwamba hana mtu mwingine anayemtegemea zaidi yangu.
“Mimi nikasema kwa kuwa ni mgonjwa ngoja niende nikamwangalie hali yake nilipofika nilimkuta hawezi kwa chochote. “Ikabidi aniombe msamaha na kaniambia kuwa, mke wangu nimejifunza kwa hili naomba msamaha na naomba urudi uweze kuniuguza na kuangalia watoto.
“Ile hali niliyoikuta pale nilishindwa kuondoka ikabidi nibaki kumuuguza na nikawa nawasiliana na mawifi zangu kama kawaida kwa ajili ya mgonjwa. “Kuna siku alizidiwa sana, ilikuwa baada ya miezi minne nikiwa namuuguza, alikuwa anahitaji kwenda chooni ikabidi nimshikilie, tukiwa tunaelekea chooni ghafla nguvu zilimuisha akanidondoka, nilipomtazama hali yake ilikuwa imebadilika nikampigia simu dereva ili aje tumpeleke hospitali; nikamtaarifu pia wifi yangu. “Hata hivyo watu walipokuja na kumwangalia wakasema ameshafariki, iliniuma sana,” alisema Tatu.

KILICHOFUATA BAADA YA MSIBA
Inaelezwa kuwa wakati msiba ukiendelea zilitokea sintofahamu nyingi ambazo nyingi kati ya hizo zilikuwa zikihusisha harakati za wanandugu kutaka kujichukulia mali mapema. Inadaiwa; moja kati ya vitu vilivyoshangaza ni uwepo wa vyeti viwili vya kifo vinavyomhusu marehemu Fakhi. Kimoja kinadaiwa kuchukuliwa na baba wa marehemu huku kingine akipewa mdogo wa marehemu aliyejulikana kwa jina la Selemani.
Aidha vyeti hivyo viwili vinadaiwa kutumika kufungua mirathi katika mahakama mbili tofauti, wanaotajwa kufanya hivyo ni baba wa marehemu na mwanaye mdogo. “Cha kushangaza nilienda kwenye ofisi ya Serikali ya Mtaa kuchukua barua ili nitambulishwe kuchukua cheti cha kifo ili tuweze kufuatilia mirathi kwa kuwa watoto wanasoma huyu mkubwa Nasra ndiyo amemaliza kidoto cha nne na anadaiwa ada na huyu mwingine yupo darasa la nne na wote wanasoma shule za kulipia na baba yao ndiyo alikuwa ana jukumu la kuwasomesha.
“Nikaambiwa baba mkwe wangu amechukua na amekwenda kufungulia mirathi katika Mahakama ya Mwanzo Ilala na shemeji yangu (Selemani) naye amekwenda fungua mirathi katika Mahakama ya Mwanzo Ukonga, nikashangaa sana. “Baadaye shemeji yangu alikuja na kusema mali ni zake ikiwemo ghorofa mbili, nyumba mbili za chini, yadi ya magari, magari sita kwa hiyo kama nataka kuendelea kuishi pale nikubali niishi naye, nimekataa.
“Kitu kingine ni kwamba baba wa marehemu ambaye ni mkwe wangu amezuia wapangaji wasilipe kodi na wala magari yasifanye kazi na amekuja na makaratasi kutoka mahakani na akayabandika hapa, yakisema yeye ndiye msimamizi wa mirathi, yaani hata sielewi cha kufanya,” alisema Tatu.
MJUMBE WA MTAA ANASEMAJE?
Naye mjumbe wa Serikali ya Mtaa huo Ramadhani Mkali alithibitisha kupokea malalamiko kutoka kwa Tatu na kwamba anamtambua kuwa ni mke wa marehemu ambapo amewahi kumshauri kuhusu matatizo yake aende ustawi wa jamii. “Alipofariki Fakhi, mkewe alikuwa hana nguvu na nafikiri kutokana na kuchanganyikiwa, baba wa marehemu na mdogo wa marehemu walikwenda kuchukua vyeti vya kifo kila mmoja kwenye eneo lake, cha kushangaza marehemu ni mmoja na vyote vinatokea Rita sasa sijajua kwa nini watu wa Rita hawakushtuka.
“Lakini katika hali ya kawaida mirathi gani inafunguliwa bila ya kuwepo kwa muhtasari wowote? Nimeambiwa kuna kiongozi hapa kwenye ofisi yetu huwa anafanya vikao vya siri bila kutushirikisha sisi jambo ambalo ni kosa,” alisema mjumbe huyo.
BABA MKWE AFUNGUKA
Baada ya jina lake kutajwa mara nyingi katika sakata hili, Amani liliamua kumtafuta baba mkwe wa Tatu ili kujua kama anakusudia kumtosa mkwewe kwenye urithi wa mali za mumewe ambapo majibu yake yalikuwa haya: “Huyo mwanamke siyo mke wa marehemu mwanangu, alikuwa mke lakini akaachika na tena siyo leo ni zamani mno,” alisema mkwe huyo huku swali la kutambua kuwa mwanaye alitoa talaka kwa Tatu akilijibu: “Sijawahi kuiona talaka yake.”
Baba huyo wa marehemu alikiri pia kuwa Tatu alikwenda kumuuguza mzazi mwenzake na kwamba hata siku marehemu alipofariki alikuwa mikononi mwake. Aidha, alipoulizwa kuhusu mwanaye Selemani naye kufungua mirathi kivyake na kudai kuwa mali za marehemu kaka yake ni zake mzee huyo alisema:
“Kwanza huyo Selemeni mimi sina radhi naye, amenipiga na kunipeleka mahakani.” Kuhusu uwepo wa habari kuwa Selemani anamshawishi shemeji yake waishi wote kwenye nyumba ya marehemu, mzee Mohamed alisema: “Kama anataka kumrithi aliyekuwa mke wa kaka yake mimi sijui kwa kuwa hajaniambia.”
SELEMANI ANENA
Baada ya kumwagiwa tuhuma nzito kuwa anataka kuishi na shemeji yake, juhudi za kumtafuta Selemani ili azungumzie suala hilo zilizaa matunda ambapo alipopatikana alisema: “Yule si mke wa kaka yangu alimwacha miaka tisa iliyopita japokuwa sikuona talaka yake, kidini inaruhusiwa kuishi naye. “Amepewa nyumba moja ya marehemu anayokaa kwa kuwa mimi ndiyo niliyemwambia arudi pale, sasa ubaya wangu uko wapi?” alihoji Selemani.