
REGINALD MENGI ni moja ya majina maarufu nchini kwa kuwa ni mmoja wa watu wenye utajiri mkubwa nchini ikiwa ni pamoja na vyombo vya habari kupitia jina la IPP Media (ITV & Radio One, East Africa Tv & EA Radio, Capital Tv & Capital Radio na The Guardian).
Jina lake linafahamika kwa makampuni yote makubwa duniani yanayotunza taarifa na takwimu za mabilionea ikiwa ni pamoja na Forbes, Financial Times, Bloomberg, n.k.
Katika miradi hiyo amewekeza Dola za Marekani milioni 550 ambazo ni sawa na Sh. trilioni 1,23.
IPP Media ni moja ya makampuni makubwa katika bara la Afrika; ina magazeti 11, stesheni za radio na televisheni tano, kampuni ya kutoa huduma za intaneti, na tovuti mbalimbali za habari, pia ana biashara nyingine kubwa ikiwa ni pamoja na kampuni pekee inayotengeneza vinywaji vya Coca Cola Tanzania inayoitwa Bonite Bottlers inayotoa soda za Sprite, Fanta, Coke, maji ya Kilimanjaro n.k. Mabango yote ya Coca Cola yaliyopo nchini yanatangaza biashara zake. Pia ana machimbo mbalimbali ya madini nchini Tanzania.
Desemba 2 mwaka huu, Mengi alihojiwa na kituo cha Televisheni Kenya cha Citizen kuhusu mafanikio yake.
1: Ulizaliwa katika familia tajiri?
“Nimetokea mahali ambapo Waswahili wanasema ‘umaskini wa kutupwa’ ndani ya moyo wangu sijui kama mimi ni tajiri, mimi ni maskini kama maskini wengine kwa sababu naamini chochote nilichonacho ni cha Mungu, wakati mwingine watu wanasahau, wanajua wamepata kila kitu kwa nguvu zao, si kweli.”
2.Kitu gani kimekufanya uwe mnyenyekevu sana?
“Matajiri katika maziko huwa hawalii ukayaona machozi lakini maskini atachimba kaburi na kukuzika atalia na utaona machozi, kwa hiyo nawapenda maskini kwa sababu ni marafiki zangu na ndiyo mahali nilipotokea.”
3.Kitabu chake cha I CAN, I MUST, I WILL?
“Ukisema naweza, akili yako itazalisha jibu lako, lakini ukisema siwezi akili yako itasema, huniheshimu, huniamini na hakuna kitakachofanikiwa. Kwa hiyo chochote kwenye haya maisha unachohitaji kufanikiwa nacho ni lazima uanze na ‘nitaweza, lazima, nitafanya'”.
5. Unaiamini falsafa hiyo?
“Kwa sababu najua imenifanyia jambo gani toka kwenye umaskini mpaka hapa nilipo wakati huu ni falsafa hii, kumwamini Mungu na kila kitu kitawezekana. Mungu alipotuumba alitupa akili yenye nguvu sana na nguvu ya kufanya chochote, fikiria kwamba kama umetumia asilimia tano kufanya haya yote, fikiri kuhusiana na asilimia hamsini, themanini, tisini, inawezekana na ndiyo tunavyotakiwa kutumia akili yetu yote lakini ndiyo hivyo sisi tuna mapungufu hatuamini kama Mungu ndiyo anatupa hiyo nguvu, watu wanakuja duniani na kusema siwezi siwezi, Mungu atatuadhibu.”
Miezi miwili iliyopita Mengi alizindua kitabu chake hicho cha ‘I CAN, I MUST, I WILL’ mjini Dodoma na mgeni rasmi alikuwa Rais wa Tanzania John Magufuli.
6.Utajiri ni kila Kitu?
“Tunafikiria kuwa na pesa nyingi ni kuwa na mafanikio au kusonga mbele, si ukweli. Unaweza ukapewa pesa zote duniani na bado ukaendelea kufeli kwa sababu hautotumia pesa kwa njia inayofaa”.
Katika biashara, hayo mafundisho yatasaidia mtu uweze kufanikiwa. Lakini tusisahau imani. Imani katika biashara ni muhimu. Kuamini kwamba ninachofanya kitafanikiwa inasaidia kutokata tamaa. Kwa Wakristo Mungu ni chanzo cha imani yao, Kwa Waislamu ni Allah, Kwa watu wengine waganga wa kienyeji ndiyo chanzo cha imani yao na inasikitisha kwamba makafiri wengine wanatumia imani za kuua na kuumiza watu wengine kama albino ili kuwapatia imani hiyo.
Naomba tuelewe kwamba kitu kikubwa ni imani. Tuamini kwamba tutaweza. Kama ni kwa kumwomba Mungu au Allah, basi tufanye hivyo sababu safari ya ujasiriamali ni ngumu na pasipo kuamini hautafanikiwa.