×

ALICHOFANYIWA MTOTO HUYU… INAUMA MPAKA BASI

DAR ES SALAAM: AMA kweli kesho si siku ya kuitegemea sana; kwa sababu hujui kitakachotokea; mtoto Issaya Merikion ‘2’ mkazi wa Mzumbe mkoani Morogoro jana ya kuzaliwa kwake ilikuwa njema, lakini sasa amekatwa mkono.

 

Ijumaa limemshuhudia Issaya akilia baada ya kupata ulemavu huo wa kudumu na limewaona pia wazazi wake wakimlilia huku wengine nao wakimsikitikia kwa kile alichofanyiwa ambacho simulizi yake inasikitisha mpaka basi.

 

Waswahili walisema: Hujafa hujaumbika; mama wa mtoto huyo aitwaye Regina Hassani, anaeleza uchungu aliokuwa nao baada ya mtoto wake kipenzi kupoteza mkono wake wa kushoto kwa kile alichodai kuwa ni makosa ya daktari aliyekuwa akimtibu.

 

TUJIKUMBUSHE

Mwezi uliopita, Issaya alipelekwa katika Hospitali Mkoa wa Morogoro akitokea Zahanati ya Mzumbe akikabiliwa na tatizo la upungufu wa damu ambako alijikuta akipata tatizo la mkono kukauka baada ya kuchomwa sindano ya kumuongezea damu. Kwa mujibu wa daktari maarufu jijini Dar es Salaam, Godfrey Chale alisema tatizo hilo linajulikana kitaalamu Dry Gangrene ambalo husababishwa na mishipa ya damu kushindwa kusafirisha damu katika utaratibu unaotakiwa.

 

Alisema inawezekana daktari aliyekuwa akimuongezea damu Issaya alitoboa mishipa inayopitisha damu safi kutoka kwenye moyo na kuacha ile inayosafirisha damu inayokwenda kwenye moyo, jambo ambalo huwenda lilileta madhara hayo ya mkono wa mtoto kunyauka.

 

Kufuatia tatizo hilo, mtoto Issaya alilazimika kupewa rufaa ya kuja jijini Dar kwa ajili ya kuangalia namna ya kumtibia huku baadhi ya madaktari wa hospitali hiyo ya Mkoa wa Morogoro wakitajwa kuwaambia wazazi wa mtoto huyo kuwa, uwezekano wa kupona upo na kwamba serikali itakuwa nyuma yao katika kumuuguza.

 

“Kwanza baadhi ya madaktari na hasa huyo aliyemchoma mwanangu sindano vibaya hawakutaka kabisa tuongee na vyombo vya habari, walikuwa wakitupa imani kuwa mtoto atapatiwa dawa na mkono wake utarudi kama kawaida.

 

“Baada ya kuona hali ya mtoto siielewi ndipo ikabidi niwasiliane na ninyi (Anakumbusha toleo la kwanza la habari ya mtoto wake iliyoandikwa na Gazeti la Uwazi la Novemba, 20-26 mwaka huu) tangu hapo nimekuwa kama adui, sipati msaada wowote kutoka katika Hospitali ya Morogoro, hata huyo daktari aliyemchoma sindano sijamuona,” alisema Regina.

 

IJUMAA LAFIKA MUHIMBILI

Kutokana na kuifuatilia habari hii tangu awali, Ijumaa lilipopata taarifa kuwa, mtoto Issaya amefanyiwa oparesheni ya kukatwa mkono ndipo lilifika Hospitali ya Muhimbili kwa ajili ya kwenda kumjulia hali. Baada ya kufika lilimkuta mtoto Issaya akiwa katika maumivu makali ambayo aliyaugulia kwa kilio kilichohuzunisha ambapo mama wa mtoto alipowaona waandishi wetu alisema kwa uchungu:

 

“Issaya amekatwa mkono jamanii.” Naye alianza kulia. “Pole sana dada, wewe mshukuru Mungu kwa yote yaliyotokea, kikubwa oparesheni imefanyika vizuri Issaya atapona,” mwandishi wetu mmoja alimfariji. “Najua atapona lakini ndiyo amekuwa kilema tena, sikumzaa hivi dada yangu, alikuwa mzima. Leo nalazimika kulea mtoto mlemavu kwa ajili ya makosa ya daktari ambaye hata kumjulia hali mwanangu ameshindwa.”

 

Dakika kadhaa zilikuwa za kuhuzunisha kutokana na kilio cha mtoto na masikitiko ya mama yake ambaye wakati wote alikuwa akimlaumu daktari anayedaiwa kuwa chanzo cha mkono wa Issaya kukatwa. Hata hivyo, baada ya maneno mengi ya faraja Regina alianza kuwasilimulia waandishi wetu hali halisi ya matibabu na changamoto anazokutana nazo hospitalini hapo.

 

“Mwanangu kafanyiwa operation ya kukatwa mkono nimejisikia vibaya sana, lakini pamoja na mateso yote ninayokutana nayo huku, wakati mwingine nakosa hata hela ya kula madaktari wa hapa wameniambia natakiwa kulipia gharama za matibabu yote aliyopewa mwanangu.

 

“Gharama za matibabu ni shilingi laki mbili ya kufanyiwa operation na kuna dawa nimeandikiwa, lakini sijajuwa ni kiasi gani mpaka sasa na ukiangalia sina hata fedha na sielewi hata huyu mtoto atatibiwa na nini?

 

“Sikuwa nimepanga kuja huku, lakini imebidi kwa sababu nahangaikia afya ya mwanangu.“Wakati natoka Morogoro niliambiwa kama mtoto akija huku Dar es Salaam atatibiwa bure kutokana na mimi sina ndugu katika mkoa huu.

 

“Wakaniambia nenda tu huyo mtoto atatibiwa bure kwa sababu ana umri chini ya miaka 5, lakini nasikitika kwamba nimeambiwa huyu mtoto anatakiwa kulipiwa matibabu, yaani hapa nahisi nachanganyikiwa.

“Sina mengi sana ya kusema ila naiomba serikali yangu, namuomba Rais Magufuli anisaidie matibabu ya mwanangu na malipo ya hizi gharama ninazodaiwa hapa hospitali, maana huzu niliyonayo ni kubwa juu ya mwanangu.

 

“Naomba pia wasamaria wema wanisaidie chochote walicho nacho ili nifanikishe kuuguza kidonda cha mwanangu na niweze kumhudumia kwa chakula pia,” alisema mama Issaya. Tangu alazwe hospitalini hapo takriban wiki tatu zilizopita simulizi ya matatizo ya Issaya imekuwa ikihuzunisha wengi ambao wamekuwa wakimtembela katika wodi ya watoto alikolazwa akipatiwa matibabu.

 

“Kwa mzazi yeyote, ukimwangalia huyu mtoto huwezi kuacha kulia, mimi hapa nimemleta mwanangu anaumwa lakini nimekuwa nikifika kwa mtoto huyo naona mwanangu ana nafuu,” alisema mama mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Joyce ambaye naye anamuuguza mwanaye hospitalini hapo.

 

MGANGA MFAWIDHI MORO AZUNGUMZA

Toka awali vyombo vyetu vya habari vimekuwa vikificha jina la hospitali anakodaiwa kuchomwa sindano Issaya kutokana na wahusika kutopatikana lakini Gazeti la Ijumaa wiki iliyopita lilifanikiwa kuzungumza na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Morogoro, Dk. Ritta Lyamuya ambapo alisema:

 

“Malalamiko hayo nimeyasikia na ni kweli kwamba mtoto huyo alilazwa hapa hospitali, lakini ni mapema mno kusema chochote kuhusu hatua na nini kilitokea; tusubiri kwanza ripoti ya madaktari wa Muhimbili.” Mbali na kukataa kuzungumzia zaidi jambo hilo Dk. Lyamuya hakukiri kuwepo kwa ahadi ya hospitali hiyo kugharamia matibabu ya Issaya kama inavyodaiwa na wazazi wa mtoto huyo.

 

WAZIRI WA AFYA ASAKWA

Kutokana na kilio cha mama wa mtoto huyo kuhusu kuiomba serikali imsaidie matibabu ya mtoto huyo, Ijumaa lilimtafuta Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ili kupata kauli ya serikali lakini hakuweza kupatikana kutokana na simu yake kuita bila kupokelewa na kwamba anaendelea kutafutwa.

 

Kwa yeyote aliyeguswa na habari hii na kutaka kumchangia chochote mtoto Issaya anaweza kuwasiliana na mama yake kwa namba 0719 777 093. Kumbuka kutoa ni moyo si utajiri.