×

NISAIDIENI NIKATWE MGUU

Peter Stewart

DAR ES SALAAM: NI mtihani mzito! Peter Stewart (31), mkazi wa Ubungo – Maziwa, jijini Dar es Salaam, yupo kwenye mateso makubwa kutokana na kidonda alichonacho mguuni mwake ambapo anawaomba Watanzania wamsadie ili uweze kukatwa.  

 

Akizungumza kwa uchungu na Risasi Jumamosi, juzi Alhamisi katika ofisi za gazeti hili, Peter anasema, amehangaika sana hospitalini kutafuta matibabu lakini hali aliyofikia, madaktari wamesema tiba pekee ni mguu wake kukatwa.

 

“Inaniuma sana, lakini sina namna, inabidi mguu wangu ukatwe. Kwa maumivu niliyonayo, naona ni bora ifanyike kama madaktari wanavyoshauri. Tatizo kubwa ni fedha, nimeambiwa zinatakiwa shilingi laki tatu (300,000) ili niweze kukatwa,” anasema Peter, huku akisisitiza Watanzania wenye moyo wa huruma wamsaidie.

 

Akisimulia chanzo cha tatizo lake, Peter alisema siku moja akiwa ametoka kwenye mihangaiko yake, maeneo ya Sinza, jijini Dar es Salaam aligongwa na gari kisha akamwagikiwa na maji ya betri ndio chanzo cha matatizo yake.

 

“Kabla ya matatizo haya, nilikuwa nafanya vibarua kwenye kazi za ujenzi. Siku ya tukio nilikuwa na rafiki zangu tumetoka kibaruani, nilikuwa navuka barabara, ghafla gari likaja kwa kasi likanigonga kisha kuniburuza barabarani, huku maji ya betri yakiruka na kunimwagikia mguuni.

 

Kwa vile nilivyoburutwa, nilipata majereha makubwa kwenye mguu wangu wa kushoto. Ulichubuka sana na kubakia ngozi nyeupe tu ya ndani,” alisema na kuongeza:

“Nilipoteza fahamu baada ya pale, nikachukuliwa na kupelekwa Hospitali ya Palestina, walipoona shida yangu ni kubwa nikakimbizwa Muhimbili. Huko nililazwa takriban wiki mbili, nikipewa dawa za kutumia ili kukausha na kusafisha kidonda.

“Baadaye nikaambiwa nirudi nyumbani, niendelee kutumia dawa. Lakini nilivyorudi tena hospitali baada ya muda, nikajulishwa kuwa natakiwa kukatwa kwa sababu mguu umeathirika pakubwa sana. Nilichanganyikiwa kwakweli. Maisha yangu yamekuwa magumu, hata kula yangu ni shida,” anasema. Anasema kutokana na ugonjwa huo, ameshindwa kuendelea kujishughulisha badala yake ameamua kuwa ombaomba sehemu mbalimbali ikiwemo kwenye mataa ya Ubungo, Dar.

 

“Kutokana na hali yangu, mama mwenye nyumba aliamua kunisitiri na kuniruhusu niendelee kuishi bila kulipa kodi hadi nitakapopata nafuu. Tatizo ni gharama za matibabu na fedha za kujikimu. Nimekuwa ombaomba mimi, nawaomba Watanzania wenzangu wanisaidie, nipo kwenye maumivu makali. Napitia magumu sana katika maisha yangu kwa sasa,” alisema Peter.

 

Kuhusu ndugu zake, Peter alisema amekuwa akiwaambia baadhi yao waliopo Morogoro, wamsaidie lakini wamekuwa wakimwambia hawana fedha hata ya kwenda kumuona.

 

KUTOA NI MOYO

Ndugu Mtanzania, hali ya Peter ni mbaya, ukimuona laivu unaweza kumwaga machozi. Ana historia ya kuhuzunisha sana kwani hana wazazi na ndugu zake hawana uwezo. Alifika jijini Dar es Salaam kwa lengo la kusaka maisha, lakini amekutana na dhahama hiyo. Usiache baraka hii ikupite. Msaidie ndugu yetu huyu, maana huijui kesho yako.

 

Kama umeguswa na mkasa wake na unahitaji kumsaidia, tafadhali fika ofisini kwetu, Sinza – Mori, jijini Dar es Salaam, tunatazamana na Wanyama Hotel. Mwulizie Mhariri wa Risasi Jumamosi.

STORI: Imelda Mtema, Risasi Jumamosi