
MABINGWA watetezi wa Ligi ya Kuu ya Wanawake inayodhaminiwa na Serengeti Lite, JKT Queens, wamezipiga bao klabu za Simba na Yanga Queens baada ya kufunga mabao mengi kwenye ligi hiyo.
Ligi ya wanawake msimu huu imeanza kwa kasi huku ushindani ukiwa ni mkubwa kutokana na sapoti ya wadhamini Serengeti Lite kuwa bega kwa bega na timu shiriki.
Katika mechi mbili ambazo JKT Queens wamecheza, wamefanikiwa kufunga mabao 15 bila yenyewe kuruhusu huku Simba yenyewe ikifunga mabao nane na wameruhusu bao moja huku Yanga Princess wakifunga bao moja na wamefungwa moja timu zote zimecheza mechi mbili kila moja.
Elizabeth Buliba ni msemaji wa JKT Queens, ameliambia Championi Jumamosi kuwa, dhamira yao ni kutoa dozi kwenye michezo yote 22 ya mashindano hayo pasipo kupoteza na kuruhusu bao hata moja.
“Sisi hatuna mzaha kabisa linapofika suala la kupambana kwa sababu tunahitaji kutetea ubingwa wetu pasipo kupoteza mchezo wowote kama ilivyokuwa msimu uliopita.
“Ila safari hii tunataka tuweke rekodi ya kufunga mabao mengi pasipo sisi kufungwa bao hata moja na ndiyo maana unaona mpaka sasa tupo kileleni kwa pointi sita na tumeshafunga mabao 15 pasipo sisi kuruhusu bao,” alisema Buliba.
Lunyamadzo Mlyuka na Issa Liponda