×

Simba Leo Chungeni Wizi wa Dakika Taifa

Kikosi cha timu ya Simba.

WAARABU ni watu wajanja sana hasa katika suala la soka. Hii inatokana na wao kuwa wamepiga hatua sana.

Unapozungumzia mafanikio ya kimpira kwa Bara la Afrika. Kaskazini ndiyo bora zaidi ukilinganisha na sehemu nyingine za bara hili wakifuatiwa na Afrika Magharibi.


Algeria, Morocco, Tunisia, Misri ndiyo zinafanya vema zaidi. Wanajua mengi kuhusiana na michuano mikubwa ya Afrika na wanajua mechi ya ugenini inachezwa vipi na mechi ya nyumbani inachezwa namna gani.

 

Uchezaji wake, unakuwa na mbinu nyingi. Mara nyingi ni sare, ukizubaa wanashinda hata kwako. Walichofanya ni kuwa na timu bora kwanza na baada ya hapo linafuatia suala la kuhakikisha wanashinda katika mbinu.

 

Mazingira ya nchi za Afrika Kaskazini ni tofauti sana na Kusini mwa Jangwa la Sahara. Kwao ni jangwa, lakini hata makuzi pia ni tofauti.

JS Saoura ya Algeria, leo inashuka dimbani kuivaa Simba katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya Makundi. Itapigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na inasubiriwa kwa hamu kubwa.

 

Mara nyingi Waafrika Waarabu wana nguvu sana, hii inatokana na nidhamu yao, maumbile kwa maana ya miili. Hivyo lazima uwe umejiandaa kinguvu kwa maana ya kupambana nao.

Aina yao ya uchezaji mpira ni pasi mojamoja na kujiamini sana. Hivyo suala la upigaji pasi wanaweza hata kupiga pasi wiki nzima bila ya kuwapokonya mpira kama hautakuwa makini kuwapa presha.

 

Waarabu ni watu wanaojiamini kwa maana ya kuujua mpira lakini wazi inaonekana JS Saoura wanajua wanakutana na moja ya timu kongwe Afrika. Simba kuwahi kuing’oa Zamalek ikiwa bingwa wa Afrika, hili limebaki katika rekodi ya nchi zote za Kaskazini na wao pia wanaheshimu ukubwa wa Zamalek. Hivyo wanajua Simba haiwezi kuwa timu laini.

 

Uchezaji wao utakuwa ni wa tahadhari kubwa. Tafadhari hiyo itatengeneza mambo mawili kwa Simba na wao wanapaswa kuyajua mapema.

Kwanza ni wizi wa muda na pili presha au hasira. Hii ni kawaida kabisa ya timu za Waarabu kwa kuwa watalinda sana na kushambulia kwa kushitukiza, ukizubaa wanatumbukiza wavuni, kazi inakuwa ngumu kwako.

 

Katika suala la kuiba muda, Simba wanapaswa kuwa makini, wasipoangalia wataambulia dakika 30 za kucheza nyingine zikiwa “zimeibiwa” na Waarabu hao.

Wana mbinu nyingi sana, za kiufundi na zile za kijinga ambazo zinaendana na wao kumzonga mwamuzi, kuchelewa kurusha mpira au kupiga faulo na kadhalika.

 

Pia kuna zile za kiufundi, wanabaki na mpira muda mwingi. Utaona wanashambulia kwa nguvu halafu, wanarudisha mpira nyuma na kuanza kuuchezea kwa pasi nyingi za taratibu wakipoza hali ya Simba kutaka kushambulia. Hii ni mbaya kwa Simba ambao wako nyumbani na wanakuwa wanataka ushindi, tena mnono.

 

Pili hiyo presha, wanajua Simba wako nyumbani na watataka kushinda. Hivyo wana-wapa presha kuanzia za maneno, kusukuma au kukanyaga makusudi. Ni wajanja sana watataka kuonyesha wao ndiyo wanaoonewa. Hivyo, Simba wanapaswa kuwa makini na mambo haya.

 

Dawa nzuri kwa Waarabu ni kuwapiga mabao angalau mawili ndani ya dakika 30 na utashangazwa. Ikiwa hivyo inakuwa rahisi kuwafunga hata mabao mengine mawili au matatu. Maana kawaida yao hawapendi kushindwa, huwa kunawa-changanya na wao kupoteza kontroo.

 

FAULO:

Hili nalo ni muhimu sana, kama nilivyoeleza awali, Waarabu wako tofauti. Wanajua ukanda wetu una watu wenye maumbo madogo na wana kasi sana, kawaida wengi wenye maumbo makubwa wanakuwa na kasi ndogo. Hivyo wanajiandaa kwa mengi.

 

Moja ni kuwa na uwezo mkubwa wa kutumia mipira iliyokufa. Simba lazima wawe makini kufanya faulo nje ya eneo la 18.

Waarabu wanahakikisha wanakuwa na wapigaji mahiri ambao wakipata nafasi moja basi hiyo inaweza kuwa fimbo ya kumaliza mchezo.

Stori: Saleh Ally, Dar es salaam