×

Fei Toto, Ajibu Wapewa Dili la Misri

Mwinyi Zahera.

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, amefichua kuwa amewaambia wachezaji wake, kiungo Feisal Salim ‘Fei Toto’ na mshambuliaji Ibrahim Ajibu kuwa wana nafasi kubwa ya kwenda kucheza nchini Misri.

 

Zahera, mwenye uraia wa DR Congo na Ufaransa, amefichua siri hiyo kufuatia wachezaji hao kuonyesha uwezo mkubwa katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa juzi Jumanne kwenye Uwanja wa Taifa, Dar na Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Akizungumza na Championi Ijumaa, Zahera alisema amewaambia wachezaji hao kama wataendelea kujituma basi watakuwa nafasi kubwa ya kuitwa kwenye timu ya taifa kwa ajili ya mchezo wa kufuzu fainali za mataifa Afrika dhidi ya Uganda kwa ajili ya kwenda Misri.

 

“Nimewaeleza wachezaji wangu, Ajibu, Feisal na wengine kwamba kuendelea kufanya kwao vizuri ndiyo kuitwa kwao kwenye timu ya taifa itakayocheza na Uganda kwa ajili ya Afcon hapa na Uganda lazima atafungwa kwa hali yoyote ili waweze kwenda Afcon nchini Misri.

 

“Unajua naona wazi Tanzania inakwenda Misri ikiwafunga Uganda na mwalimu wa timu ya taifa hawezi kuchagua timu ya taifa bila ya kuwa na wachezaji wa timu iliyokuwa juu ya wengine kwenye ligi, hivyo nimewaambia wapambane ili wakacheze Afcon, Misri kwa sababu wanayo nafasi kubwa ya kwenda,” alisema Zahera