
KOCHA Mkuu wa Bandari ya Kenya, Bernard Mwalala amefunguka kuwa, matokeo aliyoyapata jana dhidi ya Simba yatazidi kuongeza chuki dhidi yake kutokana na historia aliyoiweka wakati akiichezea Yanga.
Mwalala anashikilia rekodi ya kuipa ushindi Yanga dhidi ya Simba kipindi akiichezea klabu hiyo, baada ya Simba kutawala kwa muda mrefu kwenye michezo ambayo ilizikutanisha klabu hizo kubwa Bongo.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Mwalala amesema kuwa Simba ina kiungo imara lakini kama timu pinzani ikifanikiwa kuikamata safu hiyo basi timu nzima inaharibika na ndicho walichofanya wao.
“Simba wana timu nzuri, safu yao ya kiungo ni imara na ukifanikiwa kuikamata hiyo basi unakuwa umewamaliza, sisi tulifanya hivyo ndiyo maana tukafanikiwa kushinda. “Ushindi huu unazidi kuniongezea chuki kwa Wanasimba kwa sababu niliwafunga sana wakati nikiichezea Yanga na leo nimewatoa kwenye mashindano wakati nikiwa kocha,” alisema Mwalala.