×

Wawa Awakimbia Waandishi Uwanja – Video

BEKI kisiki wa Simba, Pascal Wawa raia wa Ivory Coast, jana Jumanne aliwakwepa waandishi wa habari wasimpige picha wala wasimfanyie mahojiano wakati kikosi kizima cha Simba kikienda Misri. Wawa alifanya tukio hilo kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere uliopo Dar es Salaam wakati wachezaji wa kikosi hicho wakishuka kwenye gari lao na kuingia ndani ya uwanja tayari kwa safari hiyo.

 

Wakati wachezaji wengine wakishuka kwenye gari na kupigwa picha, Wawa alionekana kuwa mkali na kupita njia tofauti na wenzake huku akisema kwa sauti kwamba hataki kupigwa picha wala kuzungumza na mtu. “Msinipige picha, sitaki kuzungumza na mtu sasa hivi,” alisikika Wawa.

Pascal Wawa raia wa Ivory Coast

W a k a t i Wawa akifanya hivyo, kiungo wa timu hiyo, Haruna Niyonzima aliliambia
Championi Jumatano kuwa: “Unajua katika kipindi hiki ambacho mashabiki wanatushambulia, kila mmoja hapa hataki kuzungumza na mtu.”

 

Tukio hilo la Wawa kuwakimbia waandishi linahusishwa na ishu iliyowakumba hivi karibuni baadhi ya wachezaji wa Simba akiwemo Wawa na Niyonzima kuripotiwa kutoroka kambini siku moja kabla ya mchezo wao wa nusu fainali wa michuano ya SportPesa Cup dhidi ya Bandari.

 

Katika mchezo huo, Simba ilifungwa 2-1. Jana Jumanne Simba, ilikwenda Misri kwa ajili ya mchezo wao wa Jumamosi hii wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ukiwa ni wa Kundi D katika michuano hiyo.