MSANII wa Bongo Fleva, Omary Nyembo maarufu kama Ommy DImpoz amefunguka A-Z kuhusu ugonjwa wake wa koo ulivyokuwa ukimsumbua na kusema alibakiza wiki moja tu angefariki dunia kwani madhara ya tatizo alilokuwa nalo yalikuwa makubwa na sumu ilikaribia kuingia kwenye maini.
Dimpoz ambaye alianza kuugua wiki chache baada ya kumalizika kwa harusi ya staa mwenzake ambaye pia ni swahiba wake wa karibu, Alikiba kisha kutibiwa Muhimbili kabla ya kupelekwa Afrika Kusini na baadaye Ujerumani kwa matibabu zaidi, amefunguka.
“Vipimo vya Daktari ilionekana kuna sumu nimekula au nimekunywa na ndiyo iliyoleta tatizo hilo na majibu hayo nilipata katika hospital zote nilizopita Mombasa, South Africa pamoja Ujerumani. Ninamshukuru Mungu kwa sasa naendelea vizuri maana Desemba yote haikuwa nzuri sana kwangu, nilikuwa na hali mbaya lakini nilipiga moyo konde na kumuomba Mungu nikimwambia kama uhai upo basi nitaendelea kuishi na kama hamna basi nitamshukuru.
“Wakati sijafanyiwa upasuaji wa kwanza, madaktari waliniambia upasuaji utakuwa mkubwa, hivyo wakanikupa muda wa kukaa na kujitafakari tena na nikaongea na familia yangu pamoja na wasimamizi wangu na wao waliniambia tunaimani kuwa nitatoka salama na kunisihi kufanya upasuaji na nikafanya.
“Upasuaji ulichukua saa sita mpaka kumi na moja. Madaktari walikata tumboni mpaka karibia na kifua, pia shingoni na sehemu zingine na walifanya hivyo ili kupandisha tumbo juu na vitu vingine ili kuhakikisha wananusuru maisha yangu.
“Nilivyoenda Ujerumani, walivyonicheki wakagundua ‘usaha’ umezidi na unakaribia kuingia kwenye maini na nilibakiza wiki moja tu, ningechelewa basi habari ingekuwa imeisha. Walinifanyia upasuaji wa dharula na waliniambia ingechukua saa nne lakini ilichukua saa 8, nilikaa hospital wiki tatu, nashukuru imenisaidia na kwa sasa naendelea vizuri Alhamdulillah,” amesema Dimpoz.
Kuhusu kauli ya muigizaji Steve Nyerere ambaye alifanyiwa interview na moja ya chombo cha habari na kusema Dimpoz hawezi kuimba tena kwa sababu ya hali ya ugonjwa wake, huku akiwaomba Watanzania kumuombea na kuwa naye karibu ili apate faraja na kupona, Dimpoz amesema;
“Muda mwingine tunapaswa tuzitumie vizuri hizi kamera, kama kuna kitu huna uhakika ni vizuri usikizungumze, ungeweza hata kunitafuta kwanza, ila mimi sina tatizo nae, alijikwaa tu,” amezungumza Dimpoz.