×

Namungo wawekewa mzigo mezani, waifunge Yanga

Namungo FC

UONGOZI wa timu ya Namungo, umetoa ahadi ya fedha kwa wachezaji wa timu hiyo iwapo watafanikiwa kuwafunga Yanga katika mchezo wa Kombe la FA.

 

Namungo inatarajiwa kucheza na Yanga keshokutwa Jumapili kwenye Uwanja wa Majaliwa uliopo Ruhangwa, mkoani Lindi katika mchezo wa mzunguko wa tano.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, mwenyekiti wa timu hiyo, Hassan Zidadu, alisema kuwa wamekuwa na kawaida ya kutoa motisha kwa wachezaji wao katika kila mchezo ambao utahitaji kufanyika hivyo ili kuweza kupata matokeo huku akisisitiza kuwaheshimu wapinzani wao.

 

“Sisi hii kwetu ni mechi muhimu kwa sababu kwanza tunachezea kwenye uwanja wa nyumbani lakini bado tunatambua ukubwa na uzoefu wa wapinzani wetu, japo tulishacheza nao mchezo wa kirafiki lakini hauwezi kuwa sababu.

 

“Suala la kutoa motisha kwa wachezaji wetu hilo lipo na katika mchezo huu naamini kama uongozi tutakaa na kuweza kujua tunatoa kiasi gani iwapo tutafanikiwa kushinda kwa sababu ni malengo yetu,” alisema Zidadu.

Ibrahim Mussa, Dar es Salaam