




Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akizungumza na wazazi, wanafunzi, walimu pamoja na wanakijiji wa Kwala mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mabweni mawili katika shule ya Sekondari Kwala na kuwata wanakijiji hao kuchangangia katika mradi huo ili ukamilike mapema.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha amemtaka Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dkt. Leornaald Akwilapo kufika katika shule ya Sekondari Kibaha kujionea jinsi kazi ya ukarabati ilivyo chini ya kiwango ili achukue hatua zinazostahili.
Naibu Waziri Ole Nasha ametoa agizo hilo alipofanya ziara katika shule ya sekondari Kibaha kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu inayotekelezwa katika shule hiyo.
Kiongozi huyo amesema hajarizishwa na jinsi Wakala wa Majengo Nchini (TBA) walivyofanya ukarabati wa jengo bweni pamoja na maabara ya fizikia katika shule hiyo kwani hailingani na fedha ambayo tayari imeshalipwa naserikali tangu mwaka juziwalipokabidhiwa.
“Wakala huyu alipaswa awe amejenga majengo 31 lakini mpaka sasa amekarabatimajengo mawili tu na ukiyaangalia yako chini ya kiwango huku akiwa ametumia kiasi cha shilingi milioni 400.” Amesema Ole Nasha.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri amewapongeza wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kibaha kwa kufanya vizuri katika mitihani ya kitaifa bila kujali changamoto walizonazo za miundombinu ya mabweni, madarasa pamoja na vyoo.
“Wanafunzi hawa wanachukua mchepuo wa sayansi wanahitaji kujiongezea maarifa sasa nimiambiwa shule hii ina kompyuta nne namuagiza Katibu Mkuu alete kompyuta 50 shuleni hapo ziweze kuwasaidia wanafunzi” alisisitiza Naibu Waziri.
Kwa upande wake Kaka Mkuu wa Shule hiyo Jonas Baraka amemweleza Naibu Waziri kuwa wamekuwa wakikutana na changamoto nyingi za miundombinu kwani hata ileiliyokarabatiwa kwani vyoo havipitishi maji, ubovu wa vitasa vya milango pamoja na ukosefu wa maji katika baadhi ya maeneo ya shule.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri ameonyeshwa kutoridhishwa na matumizi ya zaidi ya shilingili milioni mia moja na hamsini ziliotolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa mabweni mawili katika sekondari ya Kwala na kumagiza Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Asumpter Mshama kutuma vyombo vya ulinzi na usalama kwenda kukagua mchakato mzima uliotumika katika ujenzi wa mabweni mawili ya ya shule hiyo.
Naibu Waziri Ole Nasha yupo katika ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya shule inayofadhiliwa na Wizara ya Elimu kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) katika Mkoa wa Pwani katika wilaya za Kibaha, Kisarawe na Rufiji.
Imetolewa na: Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini,
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA