×

BREAKING: WATU 5 WAFARIKI KWA KULIPUKIWA NA PETROLI SAME

Watu watano wamefariki dunia baada ya petroli iliyokuwa ndani ya nyumba waliyokuwemo kulipuka mkoani Kilimanjaro. Licha ya waliopoteza maisha, wengine wawili wamejeruhiwa. Kamanda wa mkoani hapa, Hamisi Issah amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kubainisha chanzo kuwa ni mafuta hayo kuwekwa jikoni ambako wahusika walikuwa wanapika. Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya ya Same, Rosemary Senyamule amesema mlipuko huo umetokea usiku wa kuamkia leo, Alhamisi ya Machi 7, 2019, katika Kijiji cha Marwa.

Katika nyumba hiyo, Rosemary amesema kulikuwa na watu saba wakiwamo wanne wa familia moja ambao wote wamepoteza maisha huku wawili waliojeruhiwa wakiendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC mjini Moshi. Amesema bado wanaendelea na uchunguzi ili kubaini kama kulikuwa na biashara ya petroli katika nyumba hiyo au ilikuwepo kwa malengo mengine.

“Kulikuwa na watu saba katika nyumba hiyo na mpaka mchana wamefariki watano, wawili wanaendelea na matibabu.Polisi wamefanya uchunguzi na kesho nitapata taarifa,” amesema Rosemary.

Taarifa zaidi zinafuata hivi punde.