
KIKOSI cha Serengeti Boys leo kimemaliza michuano ya Uefa Assist kwa kupokea kipigo cha mabao 5-0 dhidi ya wenyeji Uturuki.
Mechi hiyo ilikuwa ya tatu baada ya mbili za kwanza, Serengeti Boys ilianza kwa kupokea kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Guinea na mechi ya pili ikaibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Australia waliotangulia kufunga, mara mbili.

Katika mechi ya leo, Serengeti Boys walionyesha kiwango cha chini wakitoa nafasi kwa Waturuki kucheza soka safi na la kuvutia.

Pamoja na hivyo, mabeki wa Serengeti Boys walishindwa kuwa imara na makini katika uokoaji wa mipira hasa ile ya krosi ambayo ilizaa mabao yote matatu ya mwanzo.

Pamoja na mabadiliko kadhaa yaliyofanywa na Kocha Oscar Mirambo, bado Serengeti Boys ilishindwa kuonyesha kiwango bora na kuwapa nafasi wenyeji kuendelea kutawala eneo la katikati na mwisho kujipatia mabao mengine mawili.

Baada ya mchezo huo, Mirambo amesema wameyaona makosa kadhaa yaliyofanyika na sasa ni suala la kuyafanyia kazi ili kuimarisha kikosi chao.
Na Saleh Ally, Antalya