×

JOKATE: MGENI RASMI KWENYE ‘TOKOMEZA ZIRO’ NI MAMA SAMIA

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Mkoa wa Pwani, Jokate Mwegelo, akiongea na wafanyakazi wa Global Group katika ofisi za Sinza-Mori, Dar es Salaam.

 

MKUU wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, amesema mgeni rasmi katika kampeni kabambe ya Tokomeza Ziro itakayofanyika Machi 30 mwaka huu katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam atakuwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassani.

 

Akizungumza na Global TV leo, Jokate aliwaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi siku hiyo ya Machi 30 mwaka huu kwenye kampeni hiyo kabambe inayolenga kuleta maendeleo ya elimu wilayani Kisarawe.

Meneja Mkuu wa Global Group, Abdallah Mrisho (kushoto) akiongea jambo wakati akimkaribisha Jokate kuongea na wafanyakazi.

 

Alisema kampeni hiyo inakusudia kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana wilayani Kisarawe, mkoani pwani.

 

Alisema siku hiyo kutakuwa na mambo mengi ndani ya ukumbi huo na amewaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi kwa sababu elimu ikitolewa kwa mtoto wa Kisarawe ni faida kwa taifa zima.

Meneja wa Vipindi wa Global Radio, Borry Mbaraka (kushoto) akimtambulisha Jokate katika studio za Global Radio.

 

“Tokomeza ziro ni kampeni ya kuhakikisha tunapanua elimu wilayani Kisarawe na tunaanzia kwa kujenga shule hiyo ya wasichana, niwaombe wote wenye kutaka maendeleo ya elimu wajitokeze siku hiyo pale Mlimani City,” alisema mkuu huyo wa wilaya.

 

Alibainisha kuwa moja ya vipaumbele alivyojiwekea tangu ateuliwe na Rais John  Magufuli kuongoza wilaya hiyo ni kusukuma mbele maendeleo ya elimu kwa wasichana na wavulana.

Mhariri Mtendaji wa Global Publishers, Saleh Ally (kulia) akiongea jambo wakati wa kumtembeza Jokate.

 

“Kuna changamoto nyingi kama vile mimba za utotoni kwa wasichana lakini tukijenga mabweni, tutakuwa tumepunguza tatizo kwa kiasi kikubwa,” alisema Jokate na kusisitiza kuwa ni matarajio yake kuwa siku hiyo watu wengi watajitokeza ambapo meza moja itauzwa kwa shilingi milioni moja.

Jokate akiwa na viongozi wa Global Group baada ya mahojiano yake na Global TV Online. Kutoka kushoto ni Kiongozi wa Global TV Online, Amos Nyanduku, Saleh Ally, Elvan Sambuli na Abdallah Mrisho.

PICHA NA MUSA MATEJA | GPL