×

‘Wanawake Jifunzeni Kuweka Akiba Benki’ – Samia Suluhu


MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu, amewaasa wanawake kufungua akaunti kwa ajili ya familia zao kwa kuwa wao ndiyo walezi wa watoto na familia nzima.

Samia aliyesema hayo alipokuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa akaunti maalumu ya Tabasamu kutoka  benki ya TPB uliofanyika Machi, 28 mwaka huu ambapo aliipongeza benki hiyo kwa kudhamini wanawake na kuwawekea akaunti hiyo ambayo haitakuwa na makato ya kila mwezi.

Pamoja na kuwashauri wanawake waweke akiba ya  fedha katika benki ya TPB kwa kuwa itakuwa katika mikono salama, Samia alisema pia:

“Nawapongeza TPB kwa kubuni akaunti hii maalumu itakayomwezesha mwanamke kujenga utamaduni wa kuweka hela kidogokidogo ili aweze kupata mitaji ya na kuanzisha shughuli mbalimbali za kiuchumi,” alisema.

 


Alisisitiza kwamba serikali ya awamu ya tano inatambua mchango wa wanawake ambapo lengo ni kuhakikisha nafasi ya mwanamke ambaye anatoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi na anaendelea kupewa fursa ambazo ni pamoja na huruma za kibenki zilizokuwa zinatolewa na  Benki ya Wanawake nchini (TWB).

 

Pia,  Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa benki ya TPB, Dkt. Edmund Mndolwa,  alisema benki yake iliamua kuja na wazo hilo la kuanzisha akaunti hii ya ‘Tabasamu’ ikiwa ni moja ya jitihada za kuuunga mkono juhudi za serikali zenye nia ya kusaidia katika kumkomboa mwanamke Mtanzania na kumjengea uwezo wa kujiwekea akiba ili aweze kupata mtaji.

“Akaunti hii itasaidia kumjengea kila mwanamke uwezo wa kutokuwa tegemezi pale anapohitaji fedha kwa ajili ya familia na kuinua uchumi,” alimalizia.

Stori: Neema Adrian