×

DJ Aisher Nesi Mwafrika Anayesumbua Kwa U-DJ Ulaya

Lydia Philly maarufu kama DJ Aisher.

LYDIA Philly maarufu kama DJ Aisher ambaye ni mzaliwa wa Migori, Kenya, ni mmoja wa madjs maarufu kutokana na umahiri wake wa kupiga muziki.

 

DJ Aisher mwenye makazi yake jijini Berlin nchini Ujerumani, shughuli yake kubwa ni kuhudumia wagonjwa katika Hospitali ya Vivantes Humboldt- Klinikum akiwa ni nesi, lakini kazi ya u-dj ndiyo imempa ulaji na umaarufu.

Championi Ijumaa limezungumza na DJ Aisher kwa njia ya simu ili kufahamu mengi zaidi kutoka kwake kutokana na kazi anayoifanya huko Ughaibuni.

 

Ulianza lini kazi ya u-dj?
“Niliianza kazi hii mwaka 2016 nikiwa hapa Ujerumani lakini kabla ya hapo nilikuwa napenda sana kusikiliza muziki tangu nikiwa mdogo, nikiwa shule nilipangiwa kitengo cha burudani, hivyo nikazidi kuupenda muziki.

“Nilianza kwa kupiga muziki kwenye sherehe za kuzaliwa za marafiki zangu, wakawa wananiambia ninachanganya vizuri nyimbo kwa hiyo kuanzia hapo nikaanza kazi ya DJ.

 

Nani alikuvutia katika kazi ya DJ?
“Wapo wawili, DJ Ladystars wa Ufaransa na DJ Angelo wa Marekani, wakati najivunza u-dj mwaka 2013 nilikuwa nawatafuta mitandaoni.

Ulienda lini Ujerumani?
“Ilikuwa mwaka 2010, nilifika hapa kwa ajili ya kusomea unesi, kazi ya unesi ikaja baadaye, nilikuwa nikiifanya baada ya masomo, japokuwa baadaye niliajiriwa kuwa nesi kamili.

 

Changamoto gani unakutana nazo?
“Zipo nyingi kwani Ma-DJ wa kiume ninaofanya nao kazi wengi wao wana wivu sana, nikiwa kazini na nikapiga nyimbo zangu vizuri mashabiki wakakubali wao wanachukia na kuzunguka na kukata umeme.

“Kuna muda wanaharibu mitambo makusudi ili nionenake sifai lakini kwa nguvu za Mungu napambana mpaka namaliza.

Kazi yako unafanyia wapi huko Ujerumani?
“Sina eneo maalumu la kufanyia kazi kwani mara nyingi huwa ninakodiwa, mbali na Ujerumani pia nafanya hiyo kazi katika nchi nyingine za Ulaya.


Muziki wa Tanzania unasikilizwa kwa kiasi gani?
“Wasanii Alikiba na Diamond wanaongoza kusikilizwa kuliko msanii yeyote huko Afrika Mashariki, pia Harmonize, Rayvanny na Lady Jaydee huwa wanasikilizwa.

 

“Kuna ma-dj Wazungu wamekuwa wakicheza nyimbo zao, ule wimbo wa Kadogo wa Alikiba unachezwa sana huku.

Umewahi kushinda tuzo ngapi?
“Tuzo mbili, ya kwanza nilishindanishwa na ma-dj sita wa kiume na mimi mmoja wa kike, kulikuwa na ushindani mkali lakini nilishinda, tuzo nyingine niliipata mwaka 2017 baada ya kuibuka DJ bora wa kike anayechipukia huku Ujerumani.

 

Una neno gani kwa wanaoidharau kazi ya u-dj?

“Hii kazi inalipa sana kuliko hata wanaokaa maofisini, huko Tanzania nawafahamu ma-dj wawili ambao ni DJ Mafuvu (Adolf Mawazo) na International DJ D Ommy (Omar Said).

Kitu gani ambacho hautasahau katika kazi yako?
“Kiukweli yapo mengi ambayo siwezi kuyasahau na sitasahau kamwe, siku moja hapa Berlin nilitakiwa kupiga muziki katika moja ya tamasha ambalo kuna kundi la muziki kutoka Cameroon linaloitwa EX-Maleya.

 

“Walikuja hapa kwa ajili ya tamasha hilo, ilipofika zamu yangu ya kupiga muziki kila nilipopiga muziki halisi ukawa hautoki, zikawa zinasikika kelele lakini bahati nzuri meneja wangu akanisaidia na nikaendelea, hivyo sitalisahau tukio hilo kwani kama ningekwama nisingeaminiwa kwa kuwa Wazungu siku zote wanapenda mambo yaliyonyooka.

Unafanya kazi gani nyingine?
“Mimi ni nesi ninafanya kazi katika Hospitali ya Vivantes Humboldt- Klinikum hapa Ujerumani na nimesoma kwa miaka mitatu, kwa cheti changu kilivyo ninaweza kufanya kazi katika nchi yoyote ile hapa Ulaya.

 

“Hivyo, u-dj ni kazi ambayo naifanya baada ya kutoka ofisini kwangu, u-dj nilijifunza mwenyewe kupitia mitandao, sikufundishwa na mtu yeyote.

 

“Kuhusu unesi huwa sipendi kuonyesha maisha yangu ya fani hiyo mitandaoni, ndiyo maana hata huwezi kuona kuna picha nikiwa kazini nimeiweka mtandaoni, napenda maisha yangu ya huko yabaki hukohuko.

 

Una mpango wa kuitembelea Tanzania?
“Ndiyo, mpango huo upo kwa kuwa ni ndoto yangu ya muda mrefu, nahitaji kuuona Mlima Kilimanjaro pamoja na mbuga za wanyama, pia nitatembelea nchi za Kenya, Uganda na Rwanda nikionyesha kipaji changu cha kupiga muziki na natarajia kuja Tanzania, nafikiri itakuwa Novemba 15, mwaka huu, hivyo Watanzania wajiandae kunipokea.”

 

Maisha yako binafsi yakoje?
“Familia yangu yaani ndugu zangu wapo Kenya, mimi bado ni Mkenya, sina wazazi, walifariki nikiwa bado mdogo, huku (Ujerumani) naishi peke yangu, Kenya huwa naenda mara kadhaa nikipata nafasi,” anasema DJ Aisher.

Na Johnson James, Mwanza