Rais Dkt John Magufuli, leo Jumatano, Aprili 10, 2019 ameendelea na ziara yake ya siku tatu mkoani Njombe na kubaini madudu kadhaa katika mradi wa ujnzi wa kituo kikuu cha mabasi mkoani humo kisha kulazimika kuwaita hadharani Mkurugenzi wa Halmashauri, Mkandarasi na Naibu Waziri wa Tamisemi, ili watoe maelezo ni kwanini ujenzi wa stendi kuu ya mkoa huo umechelewa kukamilika tangu mwaka 2013 hadi leo 2019.
“Nilikuwa na taarifa za watu kuidai Serikali kule Lupembe, lakini jana haraka haraka wamelipwa bilioni 70. Sasa walisubiri mpaka nije ndio walipe fedha hizo? Maana mimi ni mwanadamu siwezi kuzungukia maeneo yote ndio maana nina wasaidizi.
“Kuna watu wameaminiwa katika maeneo mbalimbali lakini hawataki kuwahudumia Watanzania. Kila kiongozi kwenye eneo lake akaanze kuchunguza mambo yaliyocheleweshwa. Tukiyatatua matatizo, Tanzania itakuwa ‘Paradise’. Maamuzi yasisubiri Rais aje.
“Watu wanalalamika kuwa Stand ya Njombe haijakamilika. Mikoa mingine stendi zao zinakamilika lakini ya Njombe bado. Mkurugenzi usijaribu kunidanganya kwasababu nimekaa Wizara ya Ujenzi kwa miaka 17.
“Naibu Waziri umeahidi kuwa stendi itakuwa imekamilika baada ya siku 20 kutoka sasa, mimi nakuongezea siku 10. Nenda ukakae nisije nikakupa presha bado ni kijana mdogo. Tarehe 10 Mei, stendi itakuwa imekamilika kwa kiwango kinachotakiwa.
“Bodi ya Wahandisi ianze kumchunguza huyu mkandarasi ‘Masasi Construction’. Nendeni mkasome vifungu vya sheria vipo vinavyoruhusu kufungwa hata miaka 3. Kama kazi ya ukandarasi huiwezi nenda hata ukavue Samaki. Kazi za ubabaishaji hakuna awamu hii.
“Watu wananichukia kuwa mimi ni mkali sana, jamani mimi ni mpole kuliko hata Askofu. Unaenda mahali kuna matatizo ya ardhi, mirathi lakini viongozi wapo. Hata suala la mauaji hapa Njombe, ndio maana RPC nilimtoa, msitafute sababu nyingine,” amesema magufuli.