×

KUKU HAKANYAGI MARUMARU

HALOOOOO eeeh sho­ga yangu mwenza­ko nam­shukuru Jalali kwa kunijalia uzima ulioni­wezesha kuonana nawe katika uga wetu huu tunaozungumzia ishu za chumbani zaidi au nako­seaaa! Baada ya wiki iliyopita kuwazungumzia wenzetu wanaoishi kama wapo du­nia ya kwao, wao chumba wanakiacha kama kilivyo, yaani usafi unakuwa shida! Mwanamke mtu mzima ukimuona msafi kuanzia kucha hadi miguu nenda chumbani kwake sasa kama hujatemea mate chini! Heee heeeiyaaaa!

Shoga mjini ujue kupaka wanja tu kila mwanaume atatamani kukuoa, upo nyonyo? Ona sasa hadi nimesahau kuwaambia kile ambacho kimenileta kwako kwa siku hii ya leo! Leo nipo na hawaa wa­nawake wenzangu ambao kwao bila kutoka nyumba­ni hawawezi, mara utasikia nakwenda kwa dada Tatu Kimara, kwa shangazi Kitunda na kwenye kicheni pati Buruguni. Kama wazazi wao wako Chanika na wao wanaishi Mbagala basi haiishi wiki bila kwenda huko, yaani wao ni safari kwa kwenda mbele na kusahau kabisa wajibu wa kutulia nyum­bani.

Shoga, ndiyo maana nikaanza na kuku hakan­yagi marumaru, kwanza atapoteza uelekeo upo? Sasa kwa tabia hiyo ya kila kukicha wewe ni kiguu na njia lazima mumeo ataku­tilia shaka na kwa ambaye hataki kupiga kelele lazima atatafuta mchepuko tu!

Atafanya hivyo kwa saba­bu kila akirudi nyumbani akitegemea utampokea, utampa pole ya kazi, utam­wandalia maji ya kuoga na chakula, anaambulia patupu,wewe haupo. Shoga yangu, kwa tabia hiyo ni rahisi mumeo kutokukuamini na kuhisi unamsaliti na mbaya zaidi ni pale inapotokea kila uki­toka nyumbani simu yako haipatikani hewani.

Kwa wewe mwenye tabia hiyo, unapaswa kuelewa kwamba heshima ya mwa­namke ni kutulia nyumbani, hata unapotoka iwe kwa safari za muhimu lakini siyo kila kukicha wewe ni kiguu na njia. Kwa leo niishie hapa ni­sije kuonekana muongeaji sana bureee! Ni mimi Anti Naa ukipenda waweza ku­niita Shangingi Mstaafu.