
HATIMAYE jeshi kamili la Simba limekamilika baada ya nyota wake wa safu ya ulinzi kuwa fiti na kujiunga na kikosi hicho ambacho kitaivaa Kagera Sugar leo Jumamosi.
Simba itakuwa na kibarua mbele ya Kagera Sugar leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera ukiwa ni mchezo wa kwanza kukutana msimu huu kwenye ligi kuu.
Nyota wa Simba ambao hawakwenda Tanga mchezo uliopita kutokana na kuwa na majeruhi ni pamoja na mabeki James Kotei, Juuko Murshid na Pascal Wawa waliopata majeraha kwenye mechi dhidi ya TP Mazembe.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, alisema kuwa wachezaji wote wa Simba kwa sasa wapo fiti na wapo Kanda ya Ziwa.
“Wachezaji wote wapo fiti, hata wale ambao walikosekana kwenye mechi iliyopita ya Coastal Union, kutokana na majeraha kwa sasa wapo fiti, wapo Kanda ya Ziwa ambako tutakuwa na mechi mfululizo.
“Maandalizi na kila kitu kuelekea kwenye mchezo wetu wa Kagera Sugar tupo fiti kuweza kupambana na kuhakikisha tunapata matokeo na kuwa kwenye nafasi nzuri zaidi,” alisema Rweyemamu.
Simba itacheza na Kagera Sugar ikiwa na pointi 60 huku wapinzani wao wakiwa na alama 36.