
RAIS John Magufuli amemaliza ziara yake ya siku mbili nchini Malawi, ambapo leo Alhamisi, Aprili 25, 2019, amezindua msimu wa mauzo ya zao la tumbaku katika eneo la Lilongwe.
Akizungumza leo katika mkutano wa hadhara, akiwa mgeni wa Rais Peter Mutharika wa Malawi, katika ziara ya siku mbili aliyoianza jana, Magufuli amesema:
“Tumefurahi sana kualikwa kwenye tukio hili, hongereni Malawi kwa kuanzisha utaratibu huu wa kuwa na siku ya uzinduzi wa msimu wa mauzo ya tumbaku. Uchumi wa nchi nyingi za Afrika ikiwemo Tanzania na Malawi tunategemea sekta ya kilimo kwani kinaongoza kwa kuchangia kwenye pato la taifa ambapo zaidi ya nusu ya watu barani Afrika wameajiriwa kwenye kilimo.”

Alisisitiza pia jinsi tumbaku inavyoingiza fedha nyingi za kigeni kwa Tanzania, kuchangia katika usalama wa chakula, ajira na mali ghafi katika sekta mbalimbali.
Pia alimpongeza Rais Mutharika kwa mageuzi aliyoyafanya kwenye kilimo nchini humo ikiwa ni pamoja na kukabili changamoto ya masoko ya mazao ya kilimo.

“Hii inatokana na nchi zetu kutegemea masoko ya kimataifa, ambapo bei hazitabiriki leo zinapanda kesho zinashuka, Wanunuzi wanapanga wanavyotaka,” alisama Magufuli.
Rais amerejea leo nchini na kuanza ziara mkoani Mbeya.