RAIS Dkt. John Magufuli amefuatilia malalamiko kuhusu mtoto aliyelawitiwa na mzee wa miaka 53 na kubaini kwamba mtu huyo alihukumiwa kifungo cha maisha na sasa yuko gerezani akitumikia adhabu hiyo.
Vilevile, ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Mbeya kushughulikia matibabu ya mtoto huyo ambaye sasa ana umri wa miaka tisa, kwani hali yake ni mbaya kutokana na kufanyiwa kitendo hicho alipokuwa na umri wa miaka sita.
Magufuli aliyasema hayo leo, Aprili 27, 2019, akihutubia wananchi wa Wilaya ya Chunya kwenye uzinduzi wa Barabara ya Chunya-Mbeya na uwekaji wa jiwe la msingi katika mradi wa barabara ya Chunya-Makongorosi uliyofanyika katika viwanja vya Sabasaba, mjini Chunya, ambapo aliyaagiza mamlaka husika kulipendekeza jina la hakimu aliyetoa hukumu hiyo kuwa miongoni mwa wale watakaoteuliwa kuwa majaji.
“Hili la ubakaji linataka kuwa ugonjwa katika maeneo haya, jana wakati wa mkutano wangu Mbeya ambapo mama Swaumu Satimani Mwalembe alieleza shida yake kwamba mtoto wake (aliyekuwa na miaka sita kipindi hicho) alilawitiwa na Idd Said Sekeni, kesi ilipoanza kukawa na ujanjaujanja, wakati mwingine akienda kwenye vyombo anawekwa ndani.
“Alikwenda kwa RC Abbas Kandoro (marehemu) ambaye aliipeleka kesi hii ikashughulikiwa vizuri. Ikamkuta hakimu anaiwa Mteite, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, akatumia sheria zote, licha ya yule mhalifu kujificha lakini hakimu aliiendesha ile kesi na akahumkumu kifungo cha maisha jela.

“Kwa sababu alihukumiwa akiwa hayupo, nimetuma watu wangu kufuatilia, wamemkuta kwenye Gereza la Luanda, na picha yake nimeletewa, anatumikia kifungo cha maisha. Nimpongze sana hakimu Mteite na ninaagiza jina la huyu hakimu lipelekwe kwenye mapendekezo kwa Jaji Mkuu, kwenye majina yatayokuja kwa ajili ya kuteuliwa ujaji na la kwake liwemo.” alisema Magufuli akiipongeza mahakama kwa hatua hiyo na kuutaka uongozi kuhakikisha matibabu ya mtoto huiyo na kumpeleka shule iwapo hakupata fursa hiyo.