
SIMBA SC ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, jana walifanikiwa kuweka rekodi ya kufunga mabao matatu ndani ya dakika 24 mbele ya klabu kubwa ambayo imewahi kutwaa ubingwa wa Europa, Sevilla ya Hispania.
Katika mchezo huo wa kirafi ki wa kimataifa uliopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar, ulioandaliwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo ya SportPesa ambayo ina udhamini katika timu hizo mbili ulishuhudiwa Sevilla ikishinda mabao 5-4.

Simba ilionekana kuwa na hamu kubwa ya kuibuka na ushindi ambapo dakika ya 9, nahodha, John Bocco alifunga bao safi akipokea pasi nzuri ya Meddie Kagere.
Baada ya kuingia kwa bao hilo, dakika ya 17, Kagere aliiongezea Simba bao la pili baada ya kuuwahi mpira uliorudishwa na beki wa Sevilla, Sergi Gomez kwa kipa wake, ambapo Kagere alimchambua kipa na kuuweka mpira wavuni kwa shuti.

Dakika ya 25, Sergio Escudero akaifunga Sevilla bao baada ya mabeki wa Simba kushindwa kuondoa hatari langoni, kisha dakika nane mbele, Bocco akaongeza bao la tatu kwa shuti kali akiwa ndani ya 18 baada ya kupokea pasi safi ya Kagere. Mwekezaji wa Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’ ambaye alikuwepo uwanjani hapo, baada ya kuingia kwa bao hilo aliinuka na kushangilia kwa nguvu huku akirukaruka.

Mpaka mapumziko, Simba ilikuwa mbele kwa mabao 3-1. Kipindi cha pili ambacho kilikuwa na mabadiliko ya wachezaji wengi kwa pande zote, ilishuhudiwa Nolito akiifungia Sevila bao dakika ya 52, kisha Clatous Chama akaongeza bao la nne kwa Simba dakika ya 62 akimalizia pasi ya Bocco.
Sevilla baada ya kufungwa mabao hayo, wakabadilika sana na kushuhudiwa Quincy Promes akifunga dakika ya 83 na dakika ya 90, kisha dakika moja kabla ya kumalizika kwa mchezo huo, Nolito alifunga bao la tano kwa Sevilla.

Mchezo huo ambao ulionekana kuvuta hisia za mashabiki wengi wa ndani na nje ya Tanzania, Simba ilicheza vizuri kipindi cha kwanza, lakini kipindi cha pili Sevilla iliyopanga ‘mziki’ ilibadilika zaidi na kuibuka na ushindi huo.
SEVILLA WAPEWA KOMBE Baada ya mchezo huo, Sevilla walikabidhiwa kombe maalumu kutoka kwa SportPesa kutokana na ushindi huo, huku Bocco akifanikiwa kuibuka mchezaji bora wa mchezo huo.
Picha Musa Mateja na Stori Wilbert Molandi – GPL