×

Polisi Dar Walivyoua Majambazi Watatu Akiwemo Mwanamke! – Video

JESHI la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam kupitia kikosi kazi cha kupambana na uhalifu, limefanikiwa kuwaua majambazi watatu akiwemo mwanamke mmoja huku wengine wawili wakichoropoka na kutokomea kusikojulikana baada ya polisi kuwawekea mtego usiku wa manane wakati wakifanya uhalifu maeneo ya Kigogo Fresh jijini humo.

 

Akizungumza na wanahabari jijini Dar jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar, Lazaro Mambosasa alisema tukio hilo lilitokea Mei 25, 2019 mwaka huu majira ya saa 8 usiku katika maeneo ya Kigogo Fresh, Mtaa wa Seremala, ambapo mbali na kuua majambazi hao, polisi walifanikiwa kukamata bastola tatu aina ya Brownie zilizofutwa namba na risasi tatu zilizopatikana eneo hilo la tukio.

 

“Awali Jeshi la Polisi lilipata taarifa kutoka kwa raia wema kuwa kuna watu watano waliopanga kuvamia nyumba ya Ally Dasan (66), mkazi wa Kigogo Fresh, ambaye mke wake aitwaye Moshi Said ni mwenyekiti na mtunza hazina wa kikundi kinachoitwa Umoja Group linalochangiana kupitia vikoba.

 

“Polisi walifika eneo la tukio saa nane usiku, baada kugundua kuwa kuna askari eneo hilo majambazi hao walianza kurusha risasi kuelekea kwa polisi.  Majambazi wawili walikimbia na watatu walipata majeraha na  baadaye walifariki dunia wakiwa njiani kupelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya matibabu,” alisema Mambosasa.

 

Aidha,  amesema polisi Dar inaendelea kuwasaka majambazi wawili waliokimbia kutoka kwenye tukio hilo, na kwamba taarifa wanazo na majina yao, hivyo hawataendela kuwa salama.

MSIKIE MAMBOSASA