
VIUNGO nyota wa Taifa Stars, Mudathir Yahya na Erasto Nyoni hawatakuwa sehemu ya kikosi cha timu hiyo kwenye mechi ya Afcon kesho dhidi ya Algeria.
Nyota hao watakosa mechi hiyo ya Stars ya mwisho katika Afcon mbele ya Algeria inayoongozwa na kiungo wa Manchester City, Riyad Mahrez kutokana na sababu mbalimbali.

Mudathir yeye atalikosa pambano hilo la Algeria kutokana na kuwa na kadi mbili za njano wakati kiraka Nyoni kwa upande wake atakosekana kutokana na kuumia kwenye mechi dhidi ya Kenya ambayo Stars ilipoteza kwa mabao 3-2.
Taarifa ambazo Spoti Xtra ambalo lipo hapa nchini Misri limezipata kutoka ndani ya kambi ya timu hiyo ni kuwa, wachezaji hao watakosa pambano hilo huku wachezaji ambao hawakucheza mechi za awali dhidi ya Senegal na Kenya wakitarajiwa kupewa nafasi kwenye mechi hiyo.
Kikosi hicho cha Stars kinachonolewa na Mnigeria Emmanuel Amunike, kwenye mechi hiyo kitaingia kikiwa na hamu ya kumaliza vyema michuano kwa ushindi baada ya kufungwa mechi mbili za awali. Stars hadi sasa hawana pointi yoyote baada ya kufungwa mechi na Senegal mabao 2-0 na Kenya 3-2.
SALAH NA JUUKO BEKI wa Uganda na Klabu ya Simba, Juuko Murshid ametanabaisha kwamba yuko fiti kabisa kupambana na nyota wa Misri, Mohammed Salah watakapokutana. Wawili hao watakutana kwenye
mechi ya mwisho ya Kundi A ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) ambayo itapigwa leo Jumapili kwenye Uwanja wa Cairo International jijini hapa.
Hadi sasa Misri wanaongoza kundi hilo wakiwa na pointi sita wakati Uganda ni wa pili na alama zao nne baada ya kushinda mechi moja na sare moja. Juuko ameliambia Spoti Xtra kwamba, hana hofu ya kupambana na Salah kutokana na awali kupambana naye kwenye mechi huko nyuma kabla ya hii ya leo.
“Tunaamini itakuwa mechi ngumu lakini mambo ya mpira hatuna hofu, sisi tupo tayari kupambana na Misri na tunachotaka bila ya kujali ni kupata ushindi. “Sina hofu kumkaba Mohammed Salah na niko tayari kwa ajili ya mechi hii,” alisema Juuko