×

BENKI KUU YASITISHA UTEUZI WA FRANK NYABUNDEGE KAMA MKURUGENZI MTENDAJI WA BENKI YA TIB

Kwa mujibu wa kifungu cha sheria namba 33(1) na 33(2) (f) cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, Benki Kuu ya Tanzania imesitisha uteuzi wa Bw. Frank  Nyabundege kama Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya TIB Corporate kuanzia tarehe 13 Julai 2019.
Benki Kuu imechukua uamuzi huu kutokana na mwenendo usioridhisha wa  benki ya TIB Corporate.
Kutokana na uamuzi huo, Benki Kuu ya Tanzania kwa mamlaka iliyopewa chini ya kifungu cha sheria namba 33(2)(b) cha sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, imemteua Bw. Fred Luvanda kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji ambaye atasimamia shughuli zote za kiutendaji za benki ya TIB Corporate.
Hatua hizi zilizochukuliwa zina lengo la kuboresha usimamizi na utendaji wa mabenki yanayomilikiwa na Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.
Benki Kuu ya Tanzania inauhakikishia umma kuwa benki ya TIB Corporate itaendelea kutoa huduma na madai yote yaliyoiva yatalipwa kama kawaida.
Benki Kuu ya Tanzania itaendelea kulinda maslahi ya wenye amana katika mabenki ili kuhakikisha sekta ya fedha inakuwa stahimilivu.
BENKI KUU YA TANZANIA
IDARA YA UHUSIANO NA ITIFAKI
13 Julai 2019