
RAIS John Magufuli leo Jumanne Julai 16, 2019, ametembelea Gereza la Butimba mkoani Mwanza ambapo amewaahidi wafungwa na maofisa wa gereza hilo kuwapatia ng’ombe watatu na magunia 15 ya mchele kwa ajili ya chakula.
Magufuli aliyesame hayo alipotembelea gereza hilo na kuzungumza na wafungwa na maofisa wa gereza waliomweleza kero zao.

“Nimegundua mambo mengi hapa hata mengine hamjayaeleza. Kuna vitendo mnavyofanyiwa hamjavisema, ninajua kuwa mnaombwa rushwa, hivyo ninaomba muamini nimeona na nimesikia, mvumilie kwani hata sisi tuliopo hapa ni wafungwa au mahabusu wa baadaye,” alisema rais baada ya kusikiliza matatizo kutoka kwa wafungwa na maofisa kadhaa.
Miongoni mwa wafungwa walioeleza kero zao, na ambaye alikuwa wa kwanza kuzungumza ni Kalikenya Nyamboge aliyesema:
“Mheshimiwa rais kuna ofisa usalama yuko huku ndani anawapa wafungwa simu halafu zikikamatwa tunanyan’ganywa vitu vyetu lakini hadi leo hajafanywa kitu chochote.
“Mheshimiwa rais huyu ofisa akupe mihuri na hizo simu uondoke nazo utajua mwenyewe utaenda kufanyia nini na ikibidi ondoka naye kwani ukifanya hivyo utakiwa umetusaidia sana na ukimuacha atanidhuru.
“Sasa hivi Jenerali Kamishna ametuletea daktari msomi na alivyofika vifo ndiyo vimepungua maana walikuwa wakikuchoma sindano wanakuua.”