×

Wanne watimka kambi ya Yanga SC Morogoro

Feisal Salum

NYOTA wanne wa kikosi cha Yanga, mapema jana Jumapili, waliondoka kambini mkoani Morogoro na kurudi jijini Dar kuanza kambi ya Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars.

 

Wachezaji hao ni Metacha Mnata, Paul Godfrey, Abdulaziz Makame na Feisal Salum ambao walikuwa kambini wakijiandaa na msimu ujao wa 2019/20, wakati Kelvin Yondani ambaye naye yupo katika kikosi cha Taifa Stars, hakuwepo kambini Morogoro kutokana na kuwa na matatizo ya kifamilia.

Taifa Stars imeanza kambi kwa ajili ya kujiandaa na michezo ya kufuzu michuano ya Chan kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani ambapo itacheza dhidi ya Kenya Julai 28, mwaka huu jijini Dar, kisha kurudiana Agosti 4 jijini Nairobi, Kenya.

 

Mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema licha ya wachezaji hao kuondoka, lakini maandalizi yao yataendelea kama kawaida.

“Wale wachezaji walioitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars, wameondoka leo (jana Jumapili) kwenda Dar kujiunga na kambi wakijiandaa na mechi dhidi ya Kenya.

 

“Kuondoka kwao ni sehemu ya kutimiza majukumu ya taifa, hivyo sisi huku tutaendelea na maandalizi yetu kama kawaida,” alisema Saleh.