
ARSENAL inaaminika imefikia muafaka wa kumsajili winga hatari wa Lille ya Ufaransa, Nicolas Pepe. Klabu inadaiwa ilikubali jana kulipa ada ya uhamisho ya kiasi cha pauni milioni 72 (Sh. bilioni 205) kwa Lille ya Ufaransa. Habari zaidi zinaeleza kuwa Arsenal ipo kwenye hatua ya mwisho ya kukamilisha usajili huo.
Arsenal wamelamba dume kwa kumpata Pepe kwani ni mfungaji na mtoa asisti mzuri. Pepe alishika nafasi ya pili kwa ufungaji kwenye Ligue 1 msimu uliopita wa 2018/19 baada ya kupachika mabao 22 na kutoa asisti 12.
Arsenal inaaminika imewapiku Napoli, ambao walikuwa wanaelekea kumnasa staa huyo wa timu ya taifa ya Ivory Coast. Kwa mujibu wa televisheni ya Sky Italia, inadaiwa Arsenal imekubali kulipa bei hiyo, ambayo itakuwa rekodi kwa klabu hiyo kufuatia matakwa ya Lille.
Arsenal inasemekana itaingia mkataba wa miaka mitano na Pepe mwenye umri wa miaka 24. Pepe atakuwa mchezaji wa nne kusajiliwa na timu hiyo baada ya Gabriel Martinelli, William Saliba na Dani Ceballos, ambaye amechukuliwa kwa mkopo kutoka Real Madrid.