
SIMBA itakamilisha ratiba ya mechi za kirafiki za kujipima nchini hapa Afrika Kusini kwa kucheza na vigogo, Orlando Pirates Jumanne. Timu hiyo maarufu ya Sauzi, inanolewa na Mserbia, Milutin Sredojevic ‘Micho’ ambaye amewahi kuwa Kocha wa Yanga na timu ya Taifa ya Uganda Cranes.
Kocha huyo anafahamika zaidi kwenye ukanda wa Afrika Mashariki kutokana St.Georges ya Ethiopia, Al Hilal na El Merreikh za Sudan pamoja na SC Villa ya Uganda.

Simba wamepanga kuitumia mechi hiyo kama fainali ya maandalizi yao kutokana na ubora wa kikosi hicho chenye mastaa wakubwa wa Afrika ambao Kocha Patrick Aussems anaamini kwamba watamsaidia kujua majumuisho ya alichofanya kwenye kambi yao.
Simba inajiandaa na mechi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Ligi Kuu Bara huku ikipania kufika mbali kwenye mashindano hayo yote kulinda hadhi ya usajili wake.