×

VIDEO: MAGUFULI AZINDUA KIWANDA CHA ‘MO’ DEWJI

 

Rais  John  Magufuli na mkewe Janeth Magufuli (wa pili kushoto), Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda (wa tatu kushoto), Mkurugenzi wa Kiwanda hicho, Mohamed Dewji, Waziri wa Viwanda Innocent Bashungwa, akikata utepe kuashiria ufunguzi wa Kiwanda cha 21 st Century Food and Packaging kilichopo jijini Dar es Salaam.

RAIS John Magufuli,  leo Agosti 1, 2019, amefungua kiwanda cha kusaga unga wa mahindi na ngano cha 21st Century Food Packaging kinachomilikiwa na kampuni za Mohamed Enterprises Limited chenye uwezo wa kusaga tani 1,540 kwa siku akisema kiwanda hicho ni miongoni mwa mihimili mikuu ya maendeleo ya kiuchumi nchini.

 

Tukiwa na viwanda vya kimkakati kwa ajili ya mazao ya kimkakati tunaweza kusindika mazao yetu na kuzalisha bidhaa zilizokamilika.  Isitoshe, viwanda vinasaidia kutengeneza ajira kwa vijana na kupunguza kiasi cha bidhaa tunazoagiza kutoka nje; sioni sababu ya kuagiza bidhaa nje ya nchi wakati nyingi zinaweza kupatikana hapa nchini,” alisema rais.

…Akionyeshwa baadhi ya bidhaa za kiwanda hicho. 

Alipongeza juhudi zinazofanywa nchini ambako ujenzi wa viwanda vipya umefikisha zaidi ya viwanda 4000 nchi nzima ambapo kiwanda hicho cha Mo kinaajiri watu 380.

 

“Kutokana na mwitikio mzuri wa ujenzi wa viwanda, tumeanza kuona mabadiliko kwenye baadhi  ambapo matumizi ya bidhaa za ndani yameongezeka. Serikali inaendelea kuzishughulikia changamoto zinazoweza kupunguza kasi ya ukuaji wa sekta hii nchini,” alisema.

Alitoa wito kwa  chuo cha ufundi cha VETA na shirika la viwanda vidogo (SIDO) kuwa na ushirikiano wa karibu ili uzalishaji wa vifaa mbalimbali uweze kuhusishwa na wajasiriamali wadogo-wadogo ma wizara ihakikishe inawaendeleza wajasiriamali hao kwani ndiyo wadau wakuu katika kukuza sekta ya viwanda.

…Akizungumza jambo na Dewji. 

Naye akizungumza kwenye hafla hiyo mfanyabiashara, Mohamed Dewji (Mo) ametoa ahadi ya kumuunga mkono Rais Magufuli kwa kuwekeza shilingi bilioni 860 katika ujenzi wa viwanda na uagizaji utakaozalisha ajira 100,000 ifikapo mwaka 2025.

…Akizungumza na  wananchi wakati wa uzinduzi. 

”Leo tunatimiza miaka 50 ya uwepo wa makampuni ya Mohamed Enterprise, tunashukuru uwepo wako Rais Magufuli tukiwa tunatimiza nusu karne.  Kampuni imeajiri Watanzania zaidi ya 30,000 mijini na vijijini,” alisema Mo ambaye kampuni yake  ina matawi mbalimbali yenye viwanda takribani 40 nchini vikiwemo viwili  vya kusaga nafaka vinavyowezesha kampuni kununua mahindi hadi tani 140,000 kwa mwaka kutoka kwa wakulima nchini.