
ASKOFU Dkt. Frederick Shoo ametangazwa mshindi usiku wa kuamkia leo dhidi ya wagombea wengine katika uchaguzi wa viongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutherani Tanzania (KKKT) ambapo ataliongoza kanisa hilo kwa kipindi kingine cha miaka minne (2019-2023).
Askofu Shoo amepata kura 144 huku mshindani wake wa karibu, Dkt. Abednego Keshomshahara akipata kura 74 kati ya kura 218 zilizopigwa katika mzunguko wa mwisho baada ya kubaki wao wawili.
Awali, katika kinyang’anyiro hicho alichuana na maaskofu wenzake wakiwemo Dkt. Steven Munga, Dkt. Abednego Keshomshahara, Blaston Gavile na Dkt. Alex Malasusa (aliyewahi kuongoza kanisa hilo katika cheo hicho kwa miaka minane).
Dkt. Shoo alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuongoza kanisa hilo Agosti mwaka 2015 baada ya kupata kura 153, dhidi ya Dkt. Munga aliyepata kura 67.