MMOJA wa pacha waliotenganishwa nchini Saudi Arabia, Anisia Benatus amefariki dunia usiku wa kuamkia leo, Jumanne, kutokana na maambukizi pamoja na kujikunja utumbo mkubwa.
Anisia alilazwa Jumamosi iliyopita katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) kutokana na kupungukiwa maji mwilini pamoja na maambukizi.
Daktari bingwa wa upasuaji wa watoto, Petronila Ngiloi amesema tangu Anisia awasili nchini Ijumaa iliyopita alikuwa akitapika huku hali yake ikionesha amedhohofika. “Tulichukua vipimo mbalimbali na kumwanzishia matibabu ya kuzuia kutapika. Vipimo vimeonesha utumbo mkubwa ulikuwa umejikunja na Jumapili tukampeleka theatre kwa upasuaji,” alisema mtaalam huyo.
Alisema hadi anatoka chumba cha upasuaji alikuwa vizuri na walimrudisha ICU ambapo hata hivyo mapigo yake ya moyo kupokea hewa safi ya Oksijeni yalikuwa hayapo vizuri na usiku wa kuamkia leo Jumanne akapoteza maisha,” alisema Ngiloi.
Kufuatia hali hiyo maiti ya mtoto huyo itasafirishwa Bukoba kwa mazishi siku ya Alhamisi. Anisia na Melnesia ambao walikuwa wameungana sehemu kubwa ya mwili waliwasili nchini Ijumaa iliyopita wakitokea Saudi Arabia ambako walikuwa wakipewa matibabu ya kuwatenganisha.