
Kwa tuliokuwa pamoja, wiki iliyopita tuliianza mada hii ya Maumivu chini ya kitovu kwa wanawake. Hili ni tatizo ambalo linahitaji umakini wa hali ya juu kuweza kulitambua na kuweza kupata tiba sahihi.
Kuna baadhi ya watu wamekuwa wakipata dalili mbalimbali za tatizo hili lakini kutokana na uelewa, wanashindwa kung’amua na kujikuta wakiishi bila kujua wanazidi kulifanya tatizo liongezeke.Hivyo basi ni vyema kujifunza hapa katika makala haya tunayoendelea nayo leo ili uweze kufahamu dalili zake na kuchukua hatua za haraka pale unapohisi dalili zozote za ugonjwa huu.
Endelea…
IELEWEKE kuwa maumivu chini ya kitovu yanayohusisha afya mbovu ya kibofu cha mkojo huambatana na mgonjwa kutoa haja ndogo kidogo sana ila mara kwa mara.
Maumivu chini ya kitovu kwa wanaume huashiria pia tatizo la tezi dume liitwalo Prostatitis yaani kuvimba kwa tezi dume. Maumivu haya hujikita kwenye shina la uume na huashiria tatizo hili hasa kama mwanaume anakwenda haja ndogo mara kwa mara nyakati za usiku na umri ukiwa unaelekea miaka 50 au zaidi.
Dalili nyingine ni kutoa haja ndogo ambayo ina kasi ndogo sana tofauti na kawaida, ikiambatana na maumivu ya kiuno na mgongo, kuvimba kwa korodani, haja ndogo inayoambatana na usaha na damu, maumivu ya uume wakati wa kufika kileleni na damu katika maji ya uzazi (semen).
Kwa wanaume, maumivu haya ya chini ya kitovu huashiria pia tatizo ambalo kitaalamu hujulikana kwa jina la Hernia ambapo waswahili tunaita ngiri.
Mwanaume anaposikia maumivu haya ya chini ya kitovu ikiambatana na maumivu ya korodani, korodani moja kupungua na nyingine kukua zaidi au zote mbili kukua au kupotea, ni dalili ya ugonjwa huu ambao huharibu ubora wa uzalishwaji wa mbegu za kiume ambazo zaweza kuzalishwa chache au ambazo hazina kasi ya kutosha kusafiri kwenye via vya uzazi vya mwanamke na hivyo mwanaume kupoteza uwezo wake wa kutungisha mimba.
Maumivu chini ya kitovu kwa wanaume kama ilivyo kwa wanawake huashiria tatizo la maambukizi katika mfumo wa haja ndogo yaani (Urinary Track Infection- U.T.I) ambapo dalili zake ni kama zile za mwanamke hapo juu.
VIPIMO NA TIBA
Vipimo na tiba vyahitajika mapema kwa wanawake na wanaume bila kuchelewa ili kuepuka madhara makubwa katika mfumo wa uzazi, mkojo na hata wa chakula. Daktari akigundua tatizo atatoa dawa na mgonjwa atapona.