×

Namna ya kugundua, kuepuka utumwa wa mapenzi-2

MARAFIKI tunakutana tena kwenye safu yetu ya kupeana mawili matatu kuhusiana na uhusiano. Bila shaka kuna mambo mengi mapya huwa unajifunza kwenye kona hii.  Leo tunaendelea na mada yetu iliyoanza wiki iliyopita, ambapo tunaangalia namna ambavyo tunaweza kuepuka utumwa wa mapenzi. Naamini wiki iliyopita kuna mambo ulijifunza. Nilimalizia kwenye kipengele cha uhusiano bila penzi la kweli, lakini sikufafanua vizuri. Kwa sababu hiyo, naomba tuanze kwenye kipengele hicho ili tuweze kwenda sawa. Karibuni sana marafiki…

UHUSIANO BILA  PENZI LA KWELI

Uhusiano wa aina hii ni ule ambao mmoja wao anakuwa hana mapenzi kwa mwezake lakini analazimisha kuwa naye kwa sababu ya kupata masilahi. Mapenzi ya aina hii siku hizi yameenea sana (hasa mijini).

Unakuta mwanamke anaamua kuwa na mwanaume fulani ingawa anajua wazi kwamba hampendi lakini kwa sababu jamaa kashaonyesha mapenzi kwake na anajua wazi anampenda, basi anakubali kwa sababu ya kupata kitu!

Tatizo linakuja pale ambapo jamaa anaamua kufunga naye ndoa moja kwa moja, mara nyingi kwanza huanza kusita lakini baada ya kufikiria kwa muda mrefu ikiwa ni pamoja na kupata ushauri kwa marafiki (wenye tamaa kama yeye) huamua kuingia katika ndoa na mwanaume ambaye hajampenda akitegemea kupata maisha mazuri.

Hii ni kwa pande zote; wanaume na wanawake! Mashugamami na mashugadadi wamejaa mijini, kazi yao ni kutafuta penzi la kweli kwa gharama yoyote. Uchunguzi unaonyesha kwamba wanawake/wanaume wa aina hiyo ni wale ambao wapo katika ndoa ambazo hawana mapenzi nazo, hivyo hutumia fedha za wenza wao kununua penzi lingine nje. Huu ni utumwa!

Wewe unayefanya hivyo, fikiria kwamba unaishi na mpenzi ambaye unajua kabisa humpendi lakini unamwongopea kwa nje. Unaishi naye kwa manyanyaso, unamtesa, humpi haki yake ya ndoa ipasavyo n.k, fahamu kwamba siku akigundua kwamba unamsaliti au akikufumania, yatakukuta makubwa.

Huna haja ya kuunyima moyo wako haki ya kuwa na yule unayempenda zaidi, mapenzi hayalazimishwi, fedha, mali na anasa zote hutafutwa na hata siku moja haziwezi kununua penzi la dhati. Anza kubadilika ndugu yangu, ondoa fikra zako mbaya na uingize ufahamu mpya utakaokuweka katika ramani ya maisha ya kibinadamu na siyo ya kinyama kama uliyo nayo sasa.

KUPENDA USIPOPEDWA!

Kundi hili ni kubwa zaidi, wapo wanaokuwa na uhusiano na wapenzi ambao hawana kabisa mapenzi nao! Wanalazimika kuwa nao kwa sababu mbalimbali; mojawapo ikiwa ni kupenda kupita kiasi huku wakitumia ushawishi wa kila aina ili nao wapendwe!

Wanafanya hivyo kwa sababu wanafahamu wazi kwamba hawapendwi. Pili ni kutokana na shinikizo, ndugu, jamaa au marafiki, kumshawishi aendelee kung’ang’ania mahali wasipopenda. Rafiki yangu mpendwa, acha kujidanganya, huwezi kubadili nyekundu kuwa njano hata siku moja, kama hakupendi achana naye, subiri yupo atakayekupenda ambaye unatakiwa kumsubiri.

SHINIKIZO LA WAZAZI

Wazazi nao kwa namna moja ama nyingine wamekuwa chanzo cha watoto kujikuta wakiishi katika ndoa ambazo zinafanana na gereza la mapenzi. Hutumia kufahamiana kwao au ushawishi wa fedha kuwalazimisha watoto kuingia katika ndoa chungu.

Maji yakishamwagika hayazoleki! Kwa wale ambao tayari wameshafunga ndoa (hasa za Kanisani) ni vigumu kutoka hivyo watajikuta wakiendelea kuteseka hadi mwisho wa maisha yao. Kinachotokea hapo mara nyingi huwa ni mmoja wao kuamua kutafuta pumziko la kweli nje ya ndoa yake, jambo ambalo ni hatari sana maana linaweza kusababisha kuleta magonjwa ndani ya ndoa.

Wazazi wanatakiwa kuwapa watoto wao nafasi ya kuchagua wenzi wawapendao, hata hivyo mzazi ana haki na wajibu wa kumshauri mwanaye kama akimuona anakuwa katika uhusiano ambao yeye kama mzazi anakuwa na mashaka nao.

Kumng’ang’aniza mwanao kuwa katika uhusiano ambao yeye haupendi ni sawa na kutaka kumharibia maisha yake, maana badala ya kufikiria maisha yake, atajikuta akifikiria jinsi alivyo katika gereza la watumwa wa mapenzi, tena akiwa amehukumiwa kifungo cha maisha! Wazazi badilikeni.

Wiki ijayo nitakuwa hapa katika sehemu ya mwisho, USIKOSE!