
MBUNGE wa Viti Maalum Kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Zainab Katimba amesema kuwa anajipanga kumng’oa Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo) katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020.

Katimba amebainisha hayo jana Jumanne, Septemba 24, 2019, wakati akifanya mahojiano maalum na radio namba moja ya mtandaoni nchini, +255 Global Radio yenye makao yake makuu, Sinza-Mori jijini Dar es Salaam.

“Mwaka 2020 inawezekana, kwa kuwa nimeishangia kwenye siasa tayari. Kwetu ni Kigoma Mjini naweza kumtoa Zitto Kabwe na inawezekana. Mimi ni kijana ninayejiamini, ninaamini nitawahudumia watu wa nyumbani.

“Mara ya kwanza nilipoingia bungeni, hadi leo, moyoni mwangu ni ile ari ya kutaka kuwatumikia Watanzania na kuwa sehemu ya kutatua changamoto za vijana wenzangu.

“Nimewapambania vijana bungeni na sasa kikwazo cha experience (ufahamu wa muda mrefu) kwa vijana kimeondolewa ili kutoa nafasi kwa vijana kupata ajira kwa urahisi.

“Viongozi wanawake wengi wamenishika mkono na wameniongoza kwenye njia nzuri hadi leo nipo hivi. Kama kijana au mwanamke unaweza kufanya chochote unachohitaji ni uthubutu tu. Watoto wa kike wanahitaji kujengewa uwezo wa kujitambua ili kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia.

“Nakushukuru chama changu CCM na Jumuiya ya UVCCM kwa kuniamini na kunipa nafasi ya uongozi, kupitia UVCCM.

“Rais Magufuli ametengeneza mazingira mazuri kwa vijana na wanawake, kuna mikopo kwenye halmashauri, naomba vijana mjitokeze kwenye mfumo wa vikundi ili kuchukua mikopo hii ambayo haina riba.

“Zaidi ya wanawake 1027 wamepatiwa mafunzo na wanakwenda kunufaika na mikopo ya halmashauri inayotolewa na serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli.

“Nawaomba sana vijana na wanawake wote waunge mkono juhudi za Rais Magufuli. Tumeona yote anayoyafanya, miradi mikubwa ya maendeleo na tunavyoelekea uchumi wa kati, pia vijana tuwe sehemu ya kuchangamkia fursa za kuwa sehemu ya maamuzi.

“Mimi ni kijana kama wengine, napenda muziki, kusoma vitabu, kuangalia movie, swimming na nipo vizuri katika eneo hilo, hasa na muziki wa Bongo Fleva na Hip Hop na msanii wangu ni Vanessa Mdee. Tusiache kuingia kwenye siasa ili tubaki walalamikaji, badala yake tujitokeze tuchukue hizi nafasi ili tuwe chachu ya kujiletea maendeleo na kujenga nchi yetu.

“Kwa wasichana wote nawaomba wamtangulize Mungu mbele, wasikate tamaa, wawe na ‘role models’ (watu wanaopenda kuwa kama wao), wajitume, wajipambanue na wahangaike, watafanikiwa tu,” alisema Katimba.