Kutoka kushoto ni wanahabari wa V.o.A; Omary Kaseko, Iddi Uwesu, Mkurugenzi wa Global Group, Eric Shigongo (katikati), Mary Mgawe na Khalid Abubakari.
WANAHABARI wa Shirika la Habari la Amerika, Voice of America (V.o.A) yenye makao yake makuu Washington D.C, Marekani wamefanya ziara ya kikazi katika ofisi za Makampuni ya Global Group zilizopo Sinza, jijini Dar es Salaam leo Jumatatu, Septemba 30, 2019.

Miongoni mwa waandishi wa V.o.A waliotembelea ni Mary Mgawe, Omary Kaseko, Iddi Uwesu na Khaled Abubakar.
Lengo la V.o.A kuzuru Global Group ilikuwa ni kukuza ushirikiano wa kiutendaji na makampuni hayo yanayomiliki televisheni ya mtandaoni, Global TV Online, +255 Global Radio, mitandao ya kijamii ya Global Publishers na magazeti ya michezo (Championi,Spoti Xtra na Betika) pamoja na magazeti pendwa ya Amani, Uwazi, Ijumaa, Risasi na Ijumaa Wikienda.

Akizungumza nao, Mkurugenzi Mtendaji wa Global Group amewapongeza wanahabari hao kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuuhabarisha umma katika mabara yote ya dunia na kuwataka waendeleze ushirikiano uliotukuka na Global Group kwa manufaa ya watu wote.
Shigongo amesema anajivunia ushirikiano huo huku akiahidi kushikamana na VoA kwa kubadilishana habari, kutoa habari zenye weledi na tija kwa umma na taifa zima na kuongeza kuwa Global TV Online ambayo ni Televisheni inayoongoza kwa ubora na kufuatiliwa na watu wengi zaidi nchini, itaendelea kutoa habari zilizo bora kwa kuzingatia sheria za nchi, maadili na kanuni za tasnia ya habari.

Mbali na kukuza ushirikiano huo, wanahabari wa V.o.A, walifika pia kwa ajili ya kujifunza namna ambavyo Global TV na Global Radio wamekuwa wakifanya kazi zao za uandishi kwa weledi jambo lionalowavutia watazamaji na wasikilizaji wao duniani kote.
Kwa sasa Global TV Online na mtandao wa www.globalpublishers.co.tz vimekuwa vikishirikiana na VoA kwa miaka mingi ikiwa ni pamoja na habari, matukio, picha na video zinazopatika kwenye mitandao hiyo ambazo zimekuwa zikitumiwa na VoA, na habari zinazorushwa na VoA zimekuwa zikitumiwa pia na Global TV Online na www.globalpublishers.co.tz.
Pia kuna vipindi na taarifa za habari (Duniani Leo, kila siku jioni) kutoka VoA ambavyo vimekuwa vikirushwa kupitia Global TV Online ikiwemo; Washington Bureau, kinachotangazwa na Sunday Shomari kila Jumanne saa 5:00 asubuhi, Shaka Extra Time cha Shaka Ssali kila Jumatano saa 5:00 asubuhi na Straight Talk of Africa cha Shaka Ssali, kila Alhamisi saa 5:00 asubuhi.