
RAIS John Magufuli amemuagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa na Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Said Mtanda, kuhakikisha wanamlipa mkazi wa Namanyere Sh. milioni 15 ndani ya siku tano kama fidia ya ng’ombe alizoibiwa baada ya mtuhumiwa aliyekiri kufanya wizi huo kukimbia baada ya kupewa dhamana ya polisi.
Mama huyo amemueleza Magufuli kuwa baada ya kuibiwa ng’ombe wake 25 walimkatama mwizi na kumfikisha polisi ambapo alikiri.
“Tulimkamata mwizi tukamfikisha polisi, siku ya pili yake tukalipana Tsh 500,000 kwa kila ng’ombe, hivyo jumla kwa ng’ombe wote 25 alipaswa kulipa Tsh milioni 12.5. Na iliamriwa asiachiwa hadi alipe pesa hizo.

“Lakini tulipokwenda siku ya tatu tukakuta ameachiwa kwa dhamana, sasa hivi ameshakimbia, nimeshafuatilia kwa DC, Takukuru hadi mkoani lakini wamerudishwa ng’ombe wawili tu,” amesema mama huyo.
DC wa Nkasi amesema alishatoa maelekezo kwa jeshi la polisi kumkamata mhalifu na mdhamini na kumfikisha mahakamani.
Aidha Rais Magufuli amesema:
“Kwa sababu hamkuchukua hatua mapema, wewe DC na RPC nawapa siku tano mmulipe huyu mama shilingi milioni 15 na za usumbufu. Kazi ya polisi mkikamata mhalifu ni kumfikisha mahakamani, wewe DC ndiye Mkuu wa Ulinzi na Usalama wa Wilaya, kama jambo lilikuwa gumu ungemtarifu Mkuu wa Mkoa au ungenipigia mimi.
“Baada ya siku tano muwe mshamwekea pesa zake kwenye akaunti yake na asaini, hakikisheni anapata ulinzi. Niwaagize Waziri wa Mambo ya Ndani (Kangi Lugola) na Waziri wa Mifugo (Luhaga Mpina) mhakikishe suala hili la wizi wa mifugo linapata ufumbuzi.
Akihutubia wananchi, Magufuli aligusia pia suala la wasichana kujazwa ujauzito na wanaume, hususani wale wanaosoma ambapo alitaka zichukuliwe hatua kali.
“Nimeshangaa kusikia mabinti wetu 229 wamepata mimba, lakini sijasikia wanaume 229 wamefikishwa kwenye vyombo vya sheria, huenda wanatafuta wengine 229 wawape mimba, DC yupo, RC yupo, DAS yupo, polisi wapo, mmeshindwa nini kuwapeleka mahakamani?
“Serikali inatoa mchango wa kutoa elimu bure, wanaume bure 229 nao wanafanya kazi zao, niwaombe ndugu zangu wana Nkasi na wana Rukwa kwa ujumla tuwaogope mabinti zetu.
“Tusiwadanganye watoto kwa fedha, eti ‘I Love you’ wakati hata mkeo humnunulii nguo, wengine wanaowapa mimba wanafunzi wana wake wawili, hawamtoshi anakimbilia mabinti wa shule. Diwani kwenye kata yako kukiwa na watoto wakapewa mimba, maana yake hutoshi.

“Katika sekta ya umeme nimeambiwa tenda zinatolewa kwa mkandarasi yuleyule kila siku badala ya kusambaza tenda kwa wakandarasi wengi ili kazi imalizike haraka, wanatoa tenda kwa mtu mmoja, RC nina imani umenisikia,” alisema Magufuli akisisitiza viongozi kumaliza matatizo na kufuata taratibu zilizopo katika utendaji kazi wao.