
UDANGANYIFU kwa ‘michepuko’ miongoni mwa wanaume wengi siku hizi ni mwingi kama ambavyo tumekuwa tukiangazia kwa wiki tatu mfululizo.
“Simu yangu imejiblock siwezi kutuma hela kwa sababu ziko kwenye simu.”
“Nimetoka kumuuguza mama yangu, nimerudi siko vizuri kifedha.”
“Ntakutumia hiyo hela kesho,” lakini hatumi kama alivyoahidi.
Ni miongoni mwa sababu ambazo zimewafanya wanawake wengi ambao walikuwa wakiendesha maisha yao kwa kutegemea kuhongwa kuachana na mategemeo hayo.
Wanaume waliokuwa wakionekana kuwa ni ‘Ma-Kassim’ wakiingia mbaa wanaagiza ‘lete kama tulivyo’ wamepungua, wengi wao jeuri ya fedha imekwisha; wamekuwa watiifu kwenye ndoa zao.
Jambo hili kama tulivyoangalia wiki liyopita ndilo lililowasukuma wanawake wengi siku hizi kuamua kujitafutia maisha ili kulinda heshima zao.
Kama alivyosema Andrew wiki iliyopita kuwa: “Haya ni mapinduzi makubwa kwa wake zetu, walikuwa wamembweteka, hawataki kufanya kazi kwa sababu walikuwa wanaletewa kila kitu, leo hii hali si shwari; nao wamelazimika kuingia mitaani kufanya biashara.”
Hata hivyo hakuna mageuzi ya kiuchumi yasiyokuwa na mtikisiko, wakati wasichana waliokuwa wakichukuliwa kama nyumba ndogo za baadhi ya ‘wapiga madili’ siku za nyuma kuathirika kwa kukosa udambwidambwi wa kuhongwa, familia za akina ‘Kassim’ waliofilisika nazo haziko salama.
Uchunguzi wa OFM unaonesha kuwa, kushuka kwa pato katika familia zilizokuwa zikiishi ‘kifalme kwa kula wanachotaka na siyo kula wanachopata nazo zimetikisika.
Migogoro mingi imeibuka kwenye ndoa; sababu kubwa ni kushuka kwa pato la familia, wanaume wengi wameanza kulia kusalitiwa na kudharauliwa na wake zao.
“Mke wangu amebadilika kabisa kitabia, tofauti na zamani, jeuri imekuwa kubwa mno kiasi kwamba nahisi amepata mwanaume nje ya ndoa.”
James (jina la utambulisho tu) mkazi wa Kimara Baruti jijini Dar es Salaam, alimwambia mmoja wa wachunguzi wetu jinsi ambavyo anahisi mke wake amebadilika kitabia.
Alipouzwa kwa nini mke kabadilika kitabia alisema: “Unajua wake zetu kipato kikishuka na mapenzi yanashuka,” alisema James akimtaja mkewe kama mwakilishi wa wanawake wote jambo ambalo si sahihi kusema “WAKE ZETU,” ni bora angesema mke wake!
Hata hivyo, uchunguzi uliowahi kufanywa awali na timu yetu ya OFM kuhusiana na SABABU ZA WANAUME KUUA WAKE ZAO KWA WIVU WA KIMAPENZI ulibaini kuwa wanaume wengi wamepoteza hadhi zao hasa baada ya wanawake kuamka kimaisha.
Hali ya wanawake wengi siku hizi kuacha tabia za kutegemea kuletewa na wanaume zimewafanya wawe majasiri jambo ambalo linachukuliwa na baadhi ya wanaume kuwa ni dharau kwao kama ambavyo James alivyojaribu kulinganisha kushuka kwake kimapato na kudharauliwa na mkewe.
Kama ambavyo tumesema mageuzi yaliyofanyika kichumi miongoni mwa wanawake na wasichana wengi kuanza harakati za kujitafutia maisha kumezua mtikisiko mkubwa kwenye familia.
“Yaani mume wangu siku hizi wivu umepita kiasi kila nikichelewa kurudi ugomvi hauishi, hata nikimwabia kuwa biashara ndiyo imenichelewesha haniamini anasema nilikuwa kwa wanaume zangu,” alisema Khadija mkazi wa Keko, Dar alipozungumza na OFM walipokuwa katika uchunguzi.
Hali halisi iliyoonekana baada ya kuchunguza kwa makini ni kuwa, wanaume wengi ambao wanawake zao wameamua kuanza kufanya biashara wamekuwa wakiteswa na mambo kadhaa muhimu.
MOJA ni ile hali ya wanawake kuacha utegemezi jambo ambalo linawafanya wanaume kujiaminisha kwamba huwenda wake zao wamepata wanaume wengine wanaowategemea tofauti na wao.
PILI; ni muda wa wanawake kuwepo nyumbani. Wengi kati ya wanawake wanaofanya biashara wamekuwa wakitoka nyumbani mapema na kurudi jioni au usiku.
Kutokuwepo nyumbani kwa saa nyingi kumewafanya baadhi ya wanaume kuwa na mawazo potofu kuwa huwenda wake zao wanatumia kisingizio cha ‘kufanya biashara’ kujihusisha na usaliti katika ndoa.
TATU; wanawake kuwa na kipato wakati mwingine kikubwa kuliko wanaume kunasababisha kuwepo kwa mashaka ya uhalali wa upatikanaji wake na wakati mwingine kuonekana kama ni ‘jeuri’ kwa wanawake.
“Nafanya biashara zangu najipatia fedha kidogo namsaidia mume wangu kuendesha maisha ya familia, lakini hatosheki, yaani kitu kidogo tu anakimbilia kusema pesa zinanipa kiburi.
“Sasa zinanipa kiburi kwani nazitumia peke yangu? Kila nikipata nahudumia familia na wakati mwingine hata yeye namnunulia nguo na mahitaji mengine,” alisema Mwanahawa mkazi wa Mbagala Rangi Tatu jijini Dar.
NNE; wanawake kutumia muda mwingi kwenye kazi na kurudi nyumbani wakiwa wamechoka na hivyo kushindwa kuwajibika ipasavyo kwenye masuala ya ndoa.
“Huyu mwanamke kuna mtu anamshika masikio, haiwezekani; mimi ananichukulia kama mtu wa ziada kwake, hata tendo la ndoa ananipa siku akijisikia, muda mwingi yeye kachoka,” Frank wa Kigamboni alilalamika.
MAKALA YATAENDELEA WIKI IJAYO USIKOSE!
Stori: Mwandishi Wetu