×

Wanaume Waongeza Safari Kukwepa Michepuko

HALI ya wanaume kuwakwepa wanawake kimapenzi ambayo tumekuwa tukiizungumzia kwa wiki kadhaa ilitufikisha mahali ambapo tuliona wanawake wengi wameamua kuachana na maisha ya kuwategemea wanaume.

 

Uchunguzi wetu umeonesha kuwa, wanaume wengi siku hizi wamezidi kuota mbawa baada ya kuandamwa na maisha ya ukata.

Tumeona shuhuda nyingi kutoka kwa wanawake zikionesha kuwa, kujitenga kwa wanaume ndiko kulikowafanya wanawake wengi kuamua kuanza maisha ya kujitafutia.

 

Kama ambavyo Waswahili husema mwenda bure si sawa na mkaa bure; jitihada za wanawake kuanza kujitafutia zimeanza kuwapa faida baadhi yao na kuondokana na maisha ya kutegemea kuwekwa michepuko na waume za watu.

Hata hivyo, hali ya wanawake kuanza kuwa wajasiriamali wadogo ni ukombozi kwao lakini kwa wanaume umegeuka kuwa utumwa ambao wengi wanaulalamikia kama tulivyoona wiki iliyopita:

 

“Huyu mwanamke kuna mtu anamshika masikio, haiwezekani; mimi ananichukulia kama mtu wa ziada kwake, hata tendo la ndoa ananipa siku akijisikia, muda mwingi yeye kachoka,” Frank wa Kigamboni alilalamika.

Uchunguzi unaonesha kuwa wanawake wanaojitafutia fedha kwa kufanya shughuli ndogondogo wamejikuta wakijitenga na masuala ya ngono na kuhudumia familia.

 

Muda mwingi wanautumia kwenye shughuli za biashara na wanaporejea nyumbani huwa wamechoka kiasi kwamba hawako tayari kutumika katika kazi nyingine za kifamilia likiwa tendo la ndoa na hivyo kuishia katika mizozo na waume zao.

 

Utafiti uliofanywa hivi karibuni na Jarida la Match’s Singles la nchini Marekani kwa kushirikiana na wataalamu wa saikolojia kutoka katika baadhi ya vyuo vikuu nchini humo, umeonesha kuwa, wanawake wenye uwezo wa kifedha hawana msukumo mkubwa wa masuala ya ngono.

 

Utafiti huo uliohusisha watu 5,000 kutoka katika Mabara kadhaa yakiwa baadhi ya nchi za Afrika kama Tunisia, Mauritius na Swaziland, umebainisha kuwa harakati za mwanamke kujikomboa kiuchumi na kifikra umebadili kabisa dhana nzima ya mapenzi kwa wapenzi na wenza.

 

Aidha, Jarida hilo limeweka wazi kuwa mabadiliko hayo hayajawafurahisha baadhi ya wanaume hususani waliokuwa wakiwatumia wanawake kingono kwa ujira wa fedha na ahadi mbalimbali.

 

“Wanawake kuwa na nguvu katika uhusiano haimaanishi wataacha kuwa na ile asili ya kike, itabaki, isipokuwa watakuwa na nafasi ya kushiriki katika kufanya maamuzi na hilo ndiyo gumu kukubaliwa na wanaume wengi, ndiyo maana wanaona imekuwa taabu kuwa nao, ” alisema Profesa Connie Shehan.

 

Alisema, mabadiliko ya usawa kwa wanawake na wanaume kwa kiasi fulani yameleta faida, kwa sababu wapo wanaume leo wanawasaidia wanawake kazi zao.

Utafiti huo pia ulibaini kuwa asilimia 90 ya wanaume walisema haki sawa kati ya jinsi hizo mbili inafanya mambo mengi kuwa magumu na kusababisha wao kunyanyasika.

 

Naye mtaalamu wa masuala ya jamii kutoka Chuo Kikuu cha Jimbo la New York Brockport, Profesa Bridges Tristan alisema, kuwepo kwa usawa wa kijinsia ikiwa ni pamoja na kufanya kazi, kumiliki mali, kulipia gharama za familia si suala linalolalamikiwa na wanaume wengi.

 

“Hapa kuna mambo mawili, asili ya mwanamke kuwa chini ya mwanaume na mwanamke mwenye nguvu ya kufanya maamuzi, lakini bado yupo chini ya mwanaume.

“Wanaume wanaona karaha kuwa na wanawake wenye nguvu, waelewa wa mambo, wanaoweza kujenga hoja, wanaojulikana ndani ya familia na nje kwa juhudi zao, bila kujali wapo chini yao au laa.

 

Alisema, linapokuja suala la mapenzi, wanawake wenye uwezo wa kifedha na upeo wa kuzitafuta, wameelekeza nguvu, akili huko na kuchukulia mapenzi kama kitu cha kawaida.

 

“Mwanamke asiyekuwa na fedha hujikuta akikubali makosa hata yasiyo yake, tofauti na anayetafuta fedha, hata kama atakubali kosa ni kwa sababu ni mwanamke ameumbwa hivyo kiasili, lakini ataendelea kufanya maamuzi mengine, hatarudi nyuma kamwe,” alisema Profesa Tristan.

 

Dayness Msama wa Mikocheni Dar, alipozungumza na OFM alisema, siku hizi wanaume wengi wanapenda kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wanawake ambao si tegemezi kwao.

“Hizo sababu zilizojaa visingizio huwahusu wanawake tegemezi lakini kama mimi nina fedha zangu mwanaume atakataa vipi kukutana na mimi?

 

“Maana uwepo wangu siyo mzigo kwake, zaidi yeye ndiyo atanufaika kwa kula, kunywa, kustarehe na wakati mwingine hata fedha ya matumizi nampa.”

Je, kwa mantiki hiyo wanaume wa “niko safarini,” wamegeuka kuwa MARIOO, yaani wanapenda kulelewa na wanawake kuliko wao kuwalea?

Usikose kujiunga nasi tena wiki ijayo kwa mwendelezo wa makala haya yenye mafunzo ya aina yake kifamilia.

STORI: OFM, DAR