×

Fahamu Madaraka ya Rais, Bunge Kikatiba

KWANZA tujiulize katiba ya nchi ni nini? Katiba ni waraka wa kisiasa unaowawezesha wananchi kujitambua kama Taifa, pia ni waraka wa kiutawala unaoelezea mgawanyo wa madaraka na majukumu ya vyombo mbalimbali vya dola.

 

Ni waraka wa kisheria unaoongoza shughuli zote kisheria ambao ndio chimbuko la sheria zote nchini na pia ni muafaka wa kitaifa juu ya namna ya kuendesha mambo katika nchi.

 

Kwa mujibu wa Ibara ya 9, lengo la katiba ni kuwezesha ujenzi wa Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar au wa chochote kati ya vyombo vyake na udugu na amani kutokana na kufuata siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, ambayo inasisitiza utekelezaji wa misingi ya kijamaa kwa kuzingatia mazingira yaliyomo katika Jamhuri ya Muungano.

 

Kwanza katiba ni lazima iwawezeshe wananchi kuridhiana kitaifa, lazima isiruhusu ubaguzi wa aina yoyote miongoni mwa raia wake na katiba ni sheria mama katika nchi, hivyo hakuna sheria inayotungwa itaruhusiwa kukinzana nayo.

Kwa mujibu wa katiba, nchi ina mihimili mitatu ambayo ni; mahakama, bunge na serikali.

 

Sifa za mtu kuwa mbunge ipo katika Ibara ya 67 (1) inaelezea kuwa mtu anaweza kuwa mbunge endapo ni raia wa Jamhuri ya Muungano na ambaye ametimiza umri wa miaka ishirini na moja na ambaye anajua kusoma na kuandika Kiswahili au Kiingereza.

Sifa za mtu kuchaguliwa kuwa rais ipo katika ibara 39; inasema kuwa mtu atachaguliwa kuwa rais kama ni raia wa kuzaliwa wa Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa Sheria ya Uraia.

 

Pia awe ametimiza umri wa miaka 40 na kuendelea, awe ni mwanachama na mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa, awe na sifa za kumwezesha kuwa mbunge au Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Katika kipindi cha miaka mitano kabla ya tarehe ya Uchaguzi Mkuu, hajawahi kutiwa hatiani katika mahakama yoyote kwa kosa lolote la kukwepa kulipa kodi yoyote ya Serikali.

 

Watu wanajiuliza, kivipi bunge linaweza mshitaki rais? Ibara 46A (2) inaipa madaraka bunge kumshtaki rais endapo ametenda vitendo ambavyo kwa ujumla vinaivunja Katiba au Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, ametenda vitendo ambavyo vinakiuka maadili yanayohusu uandikishwaji wa vyama vya siasa yaliyotajwa katika ibara ya 20(2) ya Katiba, au amekuwa na mwenendo unaodhalilisha kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano, na haitatolewa hoja ya namna hiyo ndani ya miezi kumi na miwili tangu hoja kama hiyo ilipotolewa na ikakataliwa na Bunge.

 

Mwisho wa muda wa wabunge ibara 71 imeeleza kuwa mbunge atakoma kuwa mbunge na ataacha kiti chake katika Bunge ikiwa mbunge huyo atachaguliwa kuwa rais, ikiwa mbunge atakosa kuhudhuria vikao vya mikutano ya Bunge mitatu mfululizo bila ya ruhusa ya Spika.

 

Pia ikiwa itathibitishwa kwamba amevunja masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, au ikiwa Mbunge ataacha kuwa mwanachama wa chama alichokuwemo wakati alipochaguliwa au alipoteuliwa kuwa mbunge na iwapo mbunge anachaguliwa au anateuliwa kuwa Makamu wa Rais.

 

Ibara ya 44 (1) inasema rais anaweza kutangaza kuwepo kwa hali ya vita kati ya Jamhuri ya Muungano na nchi yoyote. Ibara 45 inampa mamlaka ya kutoa msamaha kwa mtu yeyote aliyepatikana na hatia mbele ya mahakama kwa kosa lolote na anaweza kutoa msamaha huo ama bila ya masharti au kwa masharti, kwa mujibu wa sheria na Ibara 46 (1).

 

Wakati wote Rais atakapokuwa bado ameshika madaraka yake kwa mujibu wa Katiba hii, itakuwa ni marufuku kumshitaki au kuendesha mashtaka ya aina yoyote juu yake mahakamani kwa ajili ya kosa lolote la jinai.

 

Ibara ya 97 inaipa bunge madaraka ya kutunga sheria bila kuathiri masharti mengine kwenye katiba.

Katiba inasema kuwa Bunge litatumia madaraka yake ya kutunga sheria kwa kufuata utaratibu wa kujadili na kupitisha Miswada ya Sheria ambayo hatimaye itabidi ipate kibali cha rais kuwa sheria.

MAKALA: ELVAN STAMBULI