
ADA ya mtoto wa shule ya msingi shilingi milioni 30 kwa mwaka? Ndiyo, hiyo ndiyo inayomtesa staa wa sinema za Kibongo, Irene Uwoya kumsomesha mwanaye, Krish Hamad Ndikumana ambayo imeibua maswali kama yote.
Katika mahojiano na mtangazaji Zamaradi Mketema hivi karibuni, Uwoya alisema ada ya mwanaye inamfanya akose usingizi na kujikuta akihangaika mno kutafuta pesa ili mwanaye huyo asome.
Katika maelezo yake, Uwoya alisema ada ya mwanaye huyo inafikia jumla ya shilingi milioni 30 za Kitanzania kwa mwaka kwa kujumlisha gharama zote. Hata hivyo, kiasi hicho cha ada kimeibua maswali mengi na kwamba inawezekanaje mtoto wa shule ya msingi kulipiwa kiasi hicho cha pesa?
“Ada shilingi milioni 30 kwa mwaka? Hebu acheni utani..,” ilisomeka sehemu ya maoni mengi ya habari hiyo kwenye Mtandao wa YouTube.
Mshangao huo ukalazimisha gazeti hili kutafuta majibu ambapo ilibainika kuwa zipo shule za aina hiyo zinazolipa zaidi ya kiasi hicho cha pesa hadi kufikia shilingi milioni 65.
“Shule gani hiyo?” Swali lingine likafuatia… Mtoto wa Uwoya anasoma Shule ya Msingi ya Feza Boys jijini Dar ambayo uchunguzi ulionesha kuwa watoto wanaosoma shule hiyo ni wa ‘wanene’.
Mbali na shule hiyo, shule nyingine zinazotajwa kuwa ni za bei mbaya nchini Tanzania ni pamoja na Morogoro International School, International School of Moshi, Aga Khan Primary and Secondary School, Heaven of Peace Academy na Kennedy House School.
Nyingine ni St. Constantine’s International School, Iringa International School, Dar es Salaam International Academy, Braeburn International School na International School of Tanganyika. “Lakini Uwoya si anasifika kwa kula bata kwenye boti na kulipia shilingi milioni 15 kwa usiku mmoja kisha kwenda kujiachia Dubai? Kulikoni kumbe ada inamnyima usingizi?” Alihoji mtu mwingine.
Katika maelezo yake kuhusu kula bata hadi kuku wanaona wivu, Uwoya alisema; “Ukiona ninakula bata, basi ujue nimefanya kazi kubwa sana na ninastahili kula bata zaidi ya hiyo.” Hata hivyo, mbali na maswali na mjadala, baadhi ya mashabiki wake walimpongeza mno Uwoya kwa kuonesha mfano kwa kujali elimu bora kwa mwanaye.
“Hongera Uwoya kwa kujali elimu ya mwanao kwenye shule nzuri maana Ndiku (baba Krish) hayupo tena,” ilisomeka sehemu nyingine ya maoni hayo. Uwoya amemzaa Krish na Ndikumana ambaye alikuwa mwanasoka maarufu wa nchini Rwanda aliyetangulia mbele ya haki mwaka 2017
STORI: Sifael Paul, Risasi Jumamosi