
KIJANA mmoja ambaye jina lake linahifadhiwa kwa sasa, amepotea kimaajabu mwishoni mwa wiki iliyopita na kudaiwa kuwa amechukuliwa msukule, hali iliyozua kizaazaa na taharuki katika Kijiji cha Chikongo, wilayani Tandahimba, Mkoa wa Mtwara na kusababisha polisi kuvamia kijiji hicho.
Habari kutoka kijijini hapo zinadai kuwa kijana huyo alitoweka kimaajabu baada ya kuingia kwenye mtumbwi na kupotea baada ya kuvurumishwa na polisi, hata hivyo tangu siku hiyo hajaonekana ndipo kijijini kwao Chikongo ikadaiwa kuwa kuna mama (jina linahifadhiwa) amemchukua msukule.
Kutokana na kitendo hicho, baadhi ya wanakijiji walianza kumfanyia fujo mama huyo huku wengine wakitaka kumuua na kizaazaa cha vurugu kilipozidi kuwa kibaya, wasamaria wema wakapiga simu polisi kuomba msaada.
Chanzo chetu kijijini hapo kinasema baada ya dakika chake, askari polisi wa kutuliza ghasia (FFU) wakiwa na magari yao walivamia kijijini hapo na kuendesha mkong’oto wa nguvu na kusababisha kikongwe cha miaka 95, Abdallah Ausi kujeruhiwa vibaya.
“Huyu mzee alikuwa ameketi katika kibaraza cha nyumba moja kijijini hapo, FFU walipofika hawakuwa wanaangalia nani ni nani, wao walikuwa wakitoa kichapo kwa kila aliyekuwa mbele yao,” kilisema chanzo hicho.
“Hali ilitisha sana, ni kama tulikuwa kwenye vita maana mabomu ya machozi yalilipuliwa na kichapo kilitembea, kwa kweli hali ilikuwa tete,” alisema mtoa habari wetu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Kamishna Msaidizi wa Polisi, (ACP) Blasius Chatanda alithibitisha polisi kufika kijijini hapo na kutuliza ghasia.
“Ni kweli niliwatuma polisi wa kutuliza ghasia baada ya kupata taarifa za kuwepo kwa vurugu kijijini hapo zilizosababishwa na kupotea kwa kijana mmoja.
“Baadhi ya watu walikuwa wakimtuhumu mkazi mmoja mwanamke kijijini hapo kumuweka msukule mtu huyo,” alisema Kamanda Chatanda.
Akaongeza: “Kwenye kufanya oparesheni kuna uwezekano polisi wamefanya ndivyo sivyo. Vikosi vyetu hufanya doria katika ukanda huu ili kudhibiti uingiaji wa watu kutoka Msumbiji ambako kuna machafuko kutokana na uchaguzi unaoendelea.” alisema kamanda huyo.
Akifafanua zaidi, alisema siku hiyo ya tukio inayotajwa, vijana wake waliwaona vijana wanaendesha mtumbwi na walipowafuatilia wakakimbia na mmoja wao akapotea na hajaonekana hadi sasa.
“Hali hiyo ilisababisha wananchi kijijini hapo kuita waganga wa kienyeji ambapo watu walimfuata mama mmoja na kumjeruhi wakimhusisha na kupotea kwa kijana huyo, tulipopata taarifa tukaenda kutuliza ghasia na kumuokoa mama huyo na ndipo yakatokea hayo ya kujeruhiwa kwa mzee huyo,” alisema.
Naye Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamadi Masauni baada ya kupata taarifa ya kujeruhiwa kwa mzee Ausi, amemuagiza kamanda wa polisi wa mkoa kufanya uchunguzi wa tukio la kujeruhiwa mtu huyo ili polisi waliohusika wachukuliwe hatua kijeshi.
“Haiwezekani mzee kama huyo (wa miaka 95) aumizwe na si jukumu la polisi kupiga mwananchi yeyote bila sababu,” alisema Naibu Waziri Masauni na kuwahakikishia wananchi kuwa jambo hilo watalifanyia uchunguzi.
“Sioni sababu ya kutumia nguvu kubwa kwa mzee kama huyo, nakuagiza RPC hakikisha unafanya uchunguzi wa tukio hili na utakapowabaini askari waliohusika, taratibu za kijeshi zifuatwe ili iwe fundisho kwa askari wengine wanaolipaka tope jeshi letu kwa kufanya matendo kinyume na maadili ya kazi zao,” alisema Masauni aliyefanya ziara ya ghafla katika kijiji hicho.
STORI:MWANDISHI WETU, MTWARA