
FAUSTINA Charles Mfi nanga ‘Nandy’ ni binti mdogo, ambaye kwa sasa Kibongobongo anaporomosha ngoma kama zote, anaimba kwa sauti ya kumtoa nyoka pangoni. Kwa wafuatiliaji wa muziki wa Bongo Fleva, kabla ya kuibuka kwa kizazi cha kina Nandy, walikuwepo kina Mwasiti, Linah, Ray C na wengineo lakini baadaye kizazi hiki kikaanza kwenda mrama. Usisahau kabla ya kina Mwasiti, alikuwepo dada lao. Kubwa la maadui, mwanamke shupavu, komando Jide alikuwa ndiye mwenye muziki wake. Jide alikuwa Jide kwelikweli,
aliweza kusimama kushindana na wasanii wanaume na kuwakalisha. Unamkumbuka Jide yule wa Hawajui aliyofanya na MwanaFa mwaka 2015? Au nikurudishe nyuma zaidi, Jide yule wa Machozi; “Nailazimisha furaha, ingawa moyoni nina machozi, nani wa kunifuta machozi, umeondoka, umekwenda mbaaliii.”
Alifanya maajabu sana kwenye wimbo wake wa Muhogo wa Jang’ombe, au Lady Jaydee aliyekwiva kwenye Historia, ni habari nyingine. Jide yule wa Yahaya; “Yahaya unaishi wapi, kwani jina lako halisi nani yahaya eeh… maskani yako Kinondoni nyumba namba haijulikani yahaya eeh…” Hii ilidhihirisha pasi na shaka kwamba jide ni dada lao. Alikuwa akifanya shoo anafunga, watu wanakuwa wamefurika.
Alisimamiwa vyema na aliyekuwa mumewe Mtangazaji Gardner G. Habash. Alionesha msuli wake kwa aliyekuwa mwamba wa muziki, marehemu Ruge Mutahaba. Aliacha kufanya kazi na marehemu Ruge ambaye wengi waliamini kwamba asingeweza kuhimili vishindo vya fi gisufi gisu lakini mwanamke huyu shupavu alifanikiwa.
Akaanzisha mgahawa wake, akawa analeta ushindani wa hali ya juu katika anga la Bongo Fleva. Aliandaa na kufanya shoo zake kubwa ndani na nje ya Tanzania. Mafanikio kwake yalionekana dhahiri kuanzia kwenye nyumba alizojenga na hata magari ya kifahari
aliyokuwa anamiliki ikiwemo Nissan Murano. Ghafl a, mambo yakabadilika. Nandy aliibuka kama upepo akitokea kwenye Jumba lile la Vipaji Tanzania (THT). Taratibu akaanza kutoa nyimbo zake mojamoja, Watanzania wakawa wanamuelewa. Alitoa Nagusagusa, Wasiku-danganye, One Day, Kivuruge na nyingine kibao. Mwendo wake haukuwa mwepesi, watu wakawa wanazidi kumuona ananoga tu.
Akafanya vizuri kwenye majukwaa ya Fiesta, baada ya kifo cha Ruge ameendeleza moto kwa kuandaa shoo kubwa za kujaza viwanja vya mpira wa miguu. Amefanya hivyo katika mikoa tofauti, jambo ambalo si rahisi sana kwa msanii wa kike kufanya. Aliwajengea nyumba wazazi wake, na sasa anaishi kwenye lihekalu lake ambalo lipo ushuani sana. Bado anamiliki magari ya kutembelea yenye hadhi.
Usisahau balaa alilolifanya hivi karibuni huko Dubai ambapo si mara ya kwanza kushiriki tamasha maarufu kwa jina la One Africa Music Fest ambalo kimsingi Jide limekuwa likimpitia kushoto. Ni uzoefu mkubwa kwake anaoupata alipopanda kwenye tamasha hilo ambalo lilikuwa na wasanii wakali karibu wote wa Afrika. Amefanya vyema kama ilivyokuwa kwa Diamond, Wizkid na wengineo.
Hivyo basi kwa hali aliyofi kia sasa hivi Nandy, huwezi kutaja wasanii watano wa kike kutoka Bongo, halafu Nandy asiwepo kwenye hiyo orodha. Watu wameshaanza kuufuta ufalme wa jide na hata waandaaji wa shoo kubwakubwa kwa sasa nchini, wanamfi kiria zaidi yeye kuliko Jide. Maana yake, Jide asipoamka basi yawezekana akapotezwa mazima na akabaki tu kuwa historia kama wimbo wake.
Kwa moto huu alionao Nandy, kama hatabweteka ndani ya miaka mitano ijayo, atakuwa msanii wa kuogopwa zaidi Bongo ambaye anaweza kushindana na msanii yeyote mwenye mafanikio!