×

Mradi wa Maziwa Mkombozi wa Wafugaji

Profesa Elisante Ole Gabriel akizungumza wakati wa uzinduzi huo.

TANZANIA kwa kushirikiana na taasisi ya kimataifa ya uwezeshaji mifugo ya maziwa ya Land o’Lakes imezindua mradi wa miaka minne wa uzalishaji bora maziwa na kuongeza soko la bidhaa za maziwa nchini ifikapo mwaka 2024.

 

Uzinduzi wa  mradi huo ambao umefanyika Hoteli ya Sea Cliff  jijini Dar es Salaam, alihudhuriwa na mgeni rasmi, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Elisante Ole Gabriel.

Sehemu ya wadau waliohudhuria hafla hiyo.

 

Prof. Elisante amesema mradi huo unazingatia uwezeshaji kwa maafisa ugani katika mikoa 26 ya Tanzania Bara na kwamba utaanza kutekelezwa katika mikoa minne ya Dar es salaam, Pwani, Tanga na Morogoro.

 

 

Alifafanua kwamba mradi huo utazingatia kuwawezesha maafisa ugani, pembejeo na uzalishaji wenye tija hadi kufikia mahitaji ya soko la bidhaa za maziwa ndani na nje ya nchi.

 

“Mradi huu unaungwa mkono na nchi kadhaa za wahisani ikiwemo Marekani,  pia unalenga kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano ya Rais John Pombe Magufuli katika kuhakikisha nchi inakua katika uchumi wa viwanda na kujitegemea kiuchumi.

 

 

“Tanzania bado ina uzalishaji mdogo wa maziwa licha ya kuwa na idadi kubwa ya mifugo.

 

“Hivyo nawataka Watanzania kupokea mradi huu kwa mikono miwili na kuondokana na ufugaji wa kuchunga, na badala yake  kuelekea ufugaji wa kibiashara na kuiwesha nchi kuongeza thamani bidhaa za maziwa kwa mahitaji ya ndani na nje ya nchi,”alisema.

 

 

Aidha alisema kwa mujibu wa takwimu za mwaka huu Tanzania ina mifugo kadhaa wakiwemo ng’ombe milioni 30, mbuzi milioni 20.5 na kondoo million 5.5 lakini wanaotumika katika uzalishaji maziwa ni milioni mbili tu.

 

Naye mratibu wa mradi huo nchini Tanzania kutoka taasisi hiyo, Bi. Neema Mrema,  amesema mradi huo pia unatekelezwa katika nchi kadhaa barani Afrika na umeonyesha mafanikio makubwa kwa kuinua pato la wafugaji na nchi husika kwa ujumla.

 

“Taasisi hii ya kimataifa imekuwa ikitekeleza miradi hii kwa kuwawezesha maafisa ugani na pembejeo za kisasa kwa manufaa ya kuleta tija kwa ongezeko la maziwa kutoka ng’ombe mmoja  kukamuliwa  lita tano hadi 15 kwa siku,”alisema.

 

HABARI: RICHARD BUKOS

PICHA: NEEMA ADRIAN