KIKAO cha kwanza cha Mkutano wa Kwanza wa Bunge la 12 kinatarajiwa kufanyika leo jijini Dodoma baada ya kukamilika kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu.
Bunge linakutana kwa mara ya kwanza leo kutokana na kumalizika kwa uchaguzi huo uliomrejesha madarakani kwa muhula wa pili wa awamu ya tano Rais John Magufuli kutokana na ushindi wake wa kishindo wa kura milioni 12.5 dhidi ya wagombea wengine 14 wa vyama vya siasa vilivyosimamisha wagombea urais.
Moja ya kazi za kwanza za vikao vya mwanzo vya mkutano huu itakuwa ni kumchagua Spika wa Bunge, Naibu wake pamoja na kuthibitisha jina la Waziri Mkuu litakalowasilishwa mbele yao na Rais Magufuli, kama Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inavyoelekeza.
Pia baada ya kuchaguliwa Spika anatarajiwa kufanya kazi ya kuwaapisha wabunge, na inatarajiwa pia wiki hii Rais Magufuli atalizindua Bunge hili la 12, kabla halijaanza rasmi majukumu yake kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania.
Majukumu ya Bunge yametamkwa katika Ibara ya 63 (2) ya Katiba ya Nchi, ikieleza, “Sehemu ya pili ya Bunge itakuwa ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano, ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi, ya kusimamia na kuishauri Serikali ya Muungano pamoja na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake.
Bunge kama linavyofahamika na wengi, ni chombo cha wawakilishi wa wananchi. Imani kubwa iliyooneshwa na wananchi kwa wabunge hao inapaswa kuonyeshwa pia kwa wabunge kwa kuhakikisha wanatimiza majukumu yao makubwa yaliyoainishwa katika Katiba ya Tanzania, kwa nia ya kuisimamia na kuishauri serikali ili kuwaletea wananchi maendeleo.
Tunafahamu kuwa wabunge watapitishwa kufahamu majukumu yao hasa ikizingatiwa kuwa hili ni Bunge jipya baada ya Uchaguzi Mkuu, hivyo wanapaswa kufahamu mambo yote muhimu kwa majukumu yaliyo mbele, jambo ambalo litakuwa msingi mzuri katika kutekeleza majukumu hayo ili kutimiza yale waliyoyaahidi kwa wananchi.
Tunaamini watakuwa ni chachu ya kuleta maendeleo kwa Taifa kwa kuisimamia na kuishauri vizuri serikali ili itimize yote iliyoyaahidi kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025, chama kilichopewa dhamana ya kuongoza Tanzania.
Tunawatakia kila la heri wabunge wanapoanza majukumu yao mapya, lakini kubwa ni kufahamu kwamba wananchi wamewaamini hivyo wasiwaangushe na watimize wajibu wao kama inavyotakiwa ili Tanzania iendelee kupiga hatua kubwa za kimaendeleo kama tulivyoshuhudia katika miaka mitano iliyopita chini ya uongozi thabiti wa Rais Magufuli.
